Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 720.1 Zatekeleza Miradi Mkoani Mtwara
Dec 19, 2023
Bilioni 720.1 Zatekeleza Miradi Mkoani Mtwara
Mkuu wa Mkoa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza wakati wa mkutano wa Waandishi wa Habari na Mkuu wa Mkoa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri leo Desemba 19, 2023 mkoani humo.
Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa jumla ya shilingi bilioni 720.1 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Mtwara.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati wa mkutano wa Waandishi wa Habari na Mkuu wa Mkoa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri leo Desemba 19, 2023 mkoani humo.

“Mkoa wa Mtwara umefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa Watanzania kwa kipindi cha Awamu ya Sita kwa kutumia shilingi bilioni 720.1 katika Sekta ya Elimu, Afya, Maji, Nishati, Viwanda, Kilimo, Utawala na Miundombinu” amebainisha Kanali Ahmed.

Aidha ameeleza kuwa, Mkoa wa Mtwara unafanya miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Sekta binafsi ikiwemo kiwanda cha Dangote kwa kutoa vifaa vya ujenzi na kampuni za uchakataji gesi hii imefanya mkoa huo kupiga hatua kwenye uwekezaji katika sekta mbalimbali.

“Mkoa una fursa za kuvutia wawekezaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa nzuri kwa kilimo, mazingira himilivu ya kisiasa na kiuchumi, uwepo wa mazingira wezeshi kwa uwekezaji na taasisi za kifedha za kutosha kutoa huduma,” ameongeza Mkuu wa Mkoa huo.

Vilevile amebainisha kuwa, Mkoa wa Mtwara umetekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa bandari kwa zaidi ya shilingi bilioni 157, upanuzi wa uwanja wa ndege kwa zaidi ya shilingi bilioni 56 na utekelezaji wa ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini kwa zaidi ya shilingi bilioni 15.

Akizungumza kuhusu hali ya ulinzi na usalama, Mkuu wa Mkoa huo amesema kuwa “hali ya ulinzi na usalama mkoani ni shwari na matukio ya kiuhalifu yanayojitokeza yameendelea kudhibitiwa na vyombo vya dola kwa kushirikiana na raia wema.

Mkoa wa Mtwara uko kusini mwa Tanzania ambapo shughuli kuu za kiuchumi kwa Mkoa huo ni pamoja na kilimo cha mazao mbalimbali, uvuvi, ufugaji, biashara, viwanda, ujenzi, utalii, uchongaji wa vinyago, kilimo cha chumvi, madini, gesi na usafirishaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi