Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 7.5 Kuimarisha Mawasiliano Nchini
Feb 02, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Maalum – DODOMA

Serikali imelipa shilingi bilioni 7.5 kwa wakandarasi wazawa kwa lengo la kuimarisha mawasiliano nchini kujenga kilomita 409 za mkongo wa Taifa ambao kwasasa una jumla ya kilomita 7,910 huku sehemu nyingine ya fedha hizo ikitumika kwenye mradi wa anuani za makazi na postikodi kwenye Halmashauri 12.

Akizungumza jijini Dodoma leo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema miradi hiyo itasaidia kukuza biashara mtandao, matumizi ya TEHAMA na huduma ya Serikali mtandao.

“Tumeamua kuwatumia wakandarasi wa ndani ya nchi, tumeona kwamba tujenge Imani kwa wakandarasi wa ndani, tufanye kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunakamilisha kazi kwa wakati” alisema Mheshimiwa Waziri.

Pamoja na hayo, Dkt. Ndungulile amewataka wananchi kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ikiwamo vitendo vya utapeli na matusi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso amewataka wakandarasi kujitangaza kwa kufanya kazi kwa umakini na kwa wakati.

“Wakandarasi wazawa niwaombe mnapopata fursa hii itumieni vizuri ili muweze kujitangaza” alisema Mheshimiwa Kakoso.

Kwa upande wao, wakandarasi wanaotekeleza miradi hii wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwaamini huku wakiahidi kufanya kazi kwa wakati.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi