Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 64. 7 Zaboresha Miundombinu ya Elimu Rukwa
Jan 29, 2024
Bilioni 64. 7 Zaboresha Miundombinu ya Elimu Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere akizungumza wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na Mkuu wa Mkoa pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri mkoani humo
Na Jonas Kamaleki - MAELEZO

Mkoa wa Rukwa umepokea shilingi 64, 706,952,025/- kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere amebainisha hayo wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na Mkuu wa Mkoa pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri mkoani humo Jumatatu wiki hii.

"Mwaka 2021 mwezi Machi mkoa wa Rukwa ulikuwa na shule za msingi 379 ambapo shule za Serikali zilikuwa 366 na shule 13 zisizo za Serikali. Hadi kufikia mwezi Januari, 2024 shule za msingi zimeongezeka hadi kufikia 409 ambapo kati ya hizo, za Serikali ni 392 na zisizo za Serikali ni 17 sawa na ongezeko la asilimia 7.9", ameeleza Makongoro.

 Ameongeza kuwa mwaka 2021 mkoa wa Rukwa ulikuwa na shuke za sekondari 97 ambapo shule za Serikali zilikuwa 73 na Shule zisizo za Serikali ni 24, lakini kufikia mwezi Januari, 2024 mkoa huo una jumla shule za sekondari 112 na kati ya hizo, shule za Serikali ni 85 na zisizo za Serikali ni 27.

Aidha, ameongeza kuwa mkoa ulipokea kiasi cha shilingi 3,000,000,000/- kwa ajili ya ujenzi wa shule ya mkoa ya wasichana inayojengwa katika eneo la Laela katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 85.

Ameeleza kuwa mkoa ulipokea kiasi cha shilingi 14,679,637,854 kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Tawi la Rukwa ambapo panajengwa jengo la taaluma ambalo litakuwa na ofisi za wafanyakazi, vyumba vya mihadhara, maktaba na maabara.  
 
Kwa mujibu wa Makongoro Nyerere, mkoa ulipokea fedha zingine kiasi cha shilingi 348,412,790/- kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, bwalo, jiko na matundu ya vyoo katika chuo cha VETA Paramawe, na kwamba utekelezaji wa ujenzi upo katika hatua ya upauaji majengo.

Makongoro amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, mkoa ulipokea shilingi 4,272,366,548/- kwa ajili ya ujenzi wa chuo kipya cha ualimu Sumbawanga ambapo kabla ya ujenzi huo wanafunzi walikuwa wakitumia majengo ya Kanisa Katoliki Sumbawanga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi