Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 39 Kutekeleza Mradi wa Tanzania ya Kidijiti
May 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Ahmed Sagaff  

Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 39.3 kutekeleza mradi wa Tanzania ya kidijiti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 utakaoanza Julai 2022 ambao utakuza Uchumi wa Kidijitali.

Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Nape amesema fedha hizo zitatumika kujenga kituo kimoja cha kukuza taaluma na ubunifu katika TEHAMA na vituo vidogo vitano kwenye kila Kanda, kukarabati vituo 10 vya Huduma pamoja na kutekeleza programu ya uelimishaji umma kuhusu mradi.

Kazi nyingine ni kujenga mfumo wa kitaifa utakaorahisisha ukusanyaji wa takwimu za TEHAMA, kusimika mitambo kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Taifa cha Kutunzia Data (NIDC), kuwezesha ununuzi wa ‘bandwidth’ kwa ajili ya matumizi ya intaneti ya Serikali na kufanya tathmini ya kuainisha mahitaji na usanifu wa kujenga mfumo wa kuwezesha biashara mtandao.

Pamoja na hayo, Serikali itajenga minara ya mawasiliano 150 kwenye Kata 150 ili kuwezesha huduma za  mawasiliano nchini, kuwajengea uwezo wataalam wa TEHAMA nchini kwa kuwapatia watalaam 200 mafunzo ya muda mfupi na wataalam 10 mafunzo ya muda mrefu pamoja na Kufanya mapitio na kuhuisha Sera, Sheria na Kanuni za Sekta ya TEHAMA.

Aidha, Serikali itajenga, kupanua na kuboresha miundombinu iliyopo ya intaneti yenye kasi (broadband) inayomilikiwa na Serikali (GovNET) na kuunganisha taasisi 100 kwenye Miundombinu hiyo na kufikisha taasisi 390 zilizounganishwa.

Sambamba na hayo, Mhe. Nape amearifu kuwa Serikali itajenga maabara tatu kwa ajili ya kufufua (refurbishment) vifaa vya TEHAMA katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza pamoja na kuwezesha ununuzi, ugavi na ufungaji wa vifaa katika kituo kimoja kikubwa na vituo vidogo vitano vya kukuza taaluma na ubunifu katika TEHAMA.

Mpaka kukamilika kwake, mradi huu utapelekea mawasiliano kwenye maeneo mapya 763 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 111.59 kitatumika kupitia mradi huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi