Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 35 Kujenga Uwanja wa Ndege Musoma
Aug 13, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu.

Serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 35 kuboresha Uwanja wa Ndege wa Musoma uliopo mkoani Mara kwa kuweka lami na kuongeza urefu wa uwanja huo ili kuruhusu ndege kubwa na ndogo kuweza kutua.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inaeleza kuwa Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, ametanabaisha gharama hizo alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja huo.

“Tunatarajia ujenzi huu utagharimu shilingi bilioni 35 ambapo utahusisha upanuzi wa uwanja huu na uwekaji wa lami, naamini kazi hizi zikikamilika uwanja huu utakuwa wa kisasa zaidi”, amesema Chamuriho.

Aidha, Waziri Chamuriho ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na vitongoji vyake ambao watapata ajira katika mradi huo, kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri fursa watakayoipata kwa kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Khalfani Haule, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Musoma pamoja na kuchochea biashara ya utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo mkoani humo.

Ameongeza kuwa uongozi wa wilaya tayari umeupokea mradi huo na wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi kutoka Beijing kwa kumpatia eneo la kuchimba mchanga na kokoto za ujenzi.

Naye, Meneja wa Uwanja wa ndege wa Musoma, Mohammed Bakari, amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo utatumia miezi 20 ambapo ujenzi ulianza mwezi Aprili, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2022.

Bakari ameeleza kuwa ujenzi wa uwanja huo unasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi