Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 15 kutekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 135 mkoani humo.
Ametoa shukrani hizo leo Septemba 25, 2024 ofisini kwake wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya kumtambulisha Mkandarasi kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd kutoka Nchini China atakayetekeleza mradi huo.
"Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Mkoa wa Pwani unakuwa mkoa wa kimkakati kwa kuwa na nyenzo zote muhimu za kuwaletea wananchi wake maendeleo ikiwemo hili la kusambaza umeme katika maeneo ya vitongoji," amebainisha Mhe. Kunenge.
Mhe. Kunenge ameipongeza REA kwa kutekeleza Ilani ya Chama Tawala kwa vitendo na amemsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi ndani ya muda kama ilivyo katika mkataba wake.
"Utaratibu huu wa kutambulisha Wakandarasi ni mzuri, unasaidia kutoa picha halisi ya tulipotoka, tulipo sasa na tunapoelekea, hongereni sana REA," alipongeza.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme maeneo ya vijijini mkoani Pwani, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amesema Mkoa wa Pwani una jumla ya vijiji 417 ambapo vijiji 407 sawa na asilimia 98 vimeunganishwa na umeme.
Amesema vijiji 10 ambavyo havijafikishiwa umeme vipo kwenye maeneo ya delta katika Wilaya ya Kibiti (vijiji 5) na visiwa katika Wilaya ya Mkuranga (vijiji 3) na Mafia (vijiji 2).
"Vijiji hivi ambavyo bado havijapata umeme tayari mpango umeandaliwa vitafikishiwa umeme wa nishati mbadala kupitia miradi ya off-grid," alifafanua Mhandisi Olotu.
Kwa upande wa vitongoji, Mhandisi Olotu alisema Mkoa wa Pwani una jumla ya vitongoji 2,045 ambapo hadi sasa vitongoji 1,135 vimepata huduma ya umeme mbayo ni sawa na asilimia 55.6.
"Mkandarasi tunaemtambulisha leo atatekeleza mradi katika vitongoji 135 ikiwa na maana vitongoji 15 kwa kila jimbo katika majimbo yote tisa ya Mkoa wa Pwani kwa gharama ya shilingi 14,983,763,390, aidha vitongoji 775 vilivyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha,” alibainisha.
Alisema REA inatekeleza miradi kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika na kwamba utambuzi wa vitongoji hivyo vya mradi ulifanywa kwa kushirikisha Wabunge wa Majimbo yote tisa mkoani humo.
Kwa upande wake Mkandarasi alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuwa atatakeleza mradi kwa mujibu wa mkataba na kwamba maandalizi yote muhimu amekwishafanya.