Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 100 Kujenga Bandari ya Uvuvi Kilwa
May 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mbaraka Kambona, Kilwa

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Wananchi hususan wanaoishi wilayani Kilwa kuhakikisha wanajipanga kutumia vyema fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambao ujenzi wake utaanza mapema mwezi Juni mwaka huu.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo ya uvuvi lililopo wilayani Kilwa, mkoani Lindi mwishoni mwa Wiki.

Wakati akiongea na Wananchi wa Wilaya hiyo alisema, kuanza kwa ujenzi wa mradi huo kutaambatana na fursa mbalimbali ambazo zitakuwa na manufaa kwao hivyo ni vyema wananchi hao wakaanza kujiandaa ili mradi utakapoanza nao waweze kuwa sehemu ya wanufaika na sio watazamaji.

Aliongeza kwa kusema kuwa katika kuhakikisha mradi huo unajengwa na kukamilika, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutengwa kiasi cha fedha kisichopungua Shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo.

"Naomba muiamini Serikali ya Mama yetu makini, Rais Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuijenga Tanzania, huu ni mradi wake wa kielelezo, wa kimkakati na utakaoacha alama kwenye nchi hii," alisema 

Awali, akitoa taarifa ya namna Wilaya ilivyojiandaa kuhakikisha mradi huo unajengwa, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainab Kawawa alisema kuwa wameshafanya matayarisho yote kuhakikisha mradi huo unajengwa huku akiongeza kuwa wananchi ambao wanakiwa kuachia maeneo yao kupisha mradi huo wapo tayari kufanya hivyo.

"tunaamini kwamba bandari hii ya kimkakati itakapojengwa na kukamilika italeta tija kubwa kwa wavuvi na wananchi kwa  ujumla, na sisi tumeshafanya matayarisho yote ili mradi huu usikwame," alisema 

Naye, Mwananchi na Mvuvi anayefanya shughuli zake wilayani Kilwa, Bw. Suleiman Mohammed akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema ni kweli wanavuna samaki katika bahari ya Hindi lakini hawana sehemu ya uhakika ya kuuzia samaki wao kwa kuwa soko lililojengwa kwa ajili ya shughuli hiyo mpaka leo halijaanza kutumika. 

"Tunakuomba Mhe. Waziri soko hili lililojengwa lifanye kazi ili tuweze kulitumia kufanya biashara zetu," alisema Mohammed

Aidha, Waziri Ndaki aliwataka wananchi ambao wanatakiwa kuachia maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi huo wasiwe na wasiwasi,  Serikali itahakikisha kila mmoja anapata haki yake anayostahili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi