Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bil. 249.7 Zatekeleza Miradi ya Maendeleo Ruvuma
Dec 20, 2023
Bil. 249.7 Zatekeleza Miradi ya Maendeleo Ruvuma
Muonekano wa moja ya barabara mkoani Ruvuma
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi bilioni 249.7 kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji, barabara, umeme, kilimo, mifugo, utaliii na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Desemba 20, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Programu ya Tumewasikia Tumewafikia inayoendeshwa na Idara ya Habari-MAELEZO.

“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mkoa umepokea jumla ya shilingi bilioni 249.7, zikiwemo fedha za ndani shilingi bilioni 128 na fedha za nje shilingi bilioni 121.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya Elimu Afya, Barabara, Viwanja vya ndege, Bandari, Maji, Umeme, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Utalii, Viwanda na Uwezeshaji wananchi kiuchumi,” amesema Mhe. Kanali Laban.

Amesema kuwa, Mkoa wa Ruvuma ulikuwa na shule za msingi 818, na za sekondari 214,  pamoja na vyuo vya ufundi (Veta) 3. Aidha kwa sasa mkoa huo una shule za msingi 841, za sekondari 233, na  vyuo vya ufundi (Veta)  4.

Kwa upande wa huduma za afya, amesema  mkoa huo ulikuwa na hospitali za wilaya 3, vituo vya afya 15 na zahanati 100. Aidha kwa sasa mkoa una hospitali za wilaya 13, vituo vya afya 34, zahanati 301, pamoja na majengo ya EMD 4.

Ameendelea kusema, mkoa huo  ulikuwa na miradi ya maji 15, ambapo wananchi 120,000 walikuwa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Kiwango cha upatikanaji maji mijini ilikuwa asilimia 50 na vijijini ilikuwa asilimia 57. Kwa sasa kuna jumla ya miradi 35 ya maji yenye jumla ya bilioni 51.2 inayoendelea  kuhudumia zaidi ya wananchi 264,000 na vijiji 81. Kiwango cha upatikanaji maji mijini imefikia asilimia 80.95 na vijijini imefikia asilimia 68.

Mkoa una vijiji 551 kati ya hivyo vijiji 480 sawa na asilimia 87.1 vimefikiwa na umeme katika Miradi ya REA na Vijiji 71 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya 3 Mzunguko wa pili kwa gharama ya shilingi Bilioni 99.6.

“Uhamasishaji umefanyika kupitia “Royal Tour” na mpango Mkakati umeandaliwa ambapo maeneo ya vivutio yamefanyiwa maboresho kwa kupeleka wanyama katika kisiwa cha Lundo na kuletwa boti kwa ajili ya kuwapeleka watalii katika kisiwa cha Lundo na Mbambabay,” amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa.

Vilevile mkoa huo, unatekeleza miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo, ujenzi wa barabara ya Mbinga Mbambabay kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 66 kwa kwa gharama ya shilingi bilioni 129.3, ujenzi wa barabara ya Amani Makoro - Ruanda (kilometa 35) kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 60.481.
 
Miradi mingine ni ukarabati na ujenzi wa Kiwanja Cha Ndege Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 37.09 pamoja na ujenzi wa Bandari kubwa na ya kisasa ya Ndumbi katika ziwa Nyasa kwa gharama ya shilingi bilioni 12.2.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi