Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bidhaa Mpya ya Afya Bima Nafuu kwa Wateja Wapatao Milioni 17.5
Dec 09, 2023
Bidhaa Mpya ya Afya Bima Nafuu kwa Wateja Wapatao Milioni 17.5
Wawakilishi kutoka kampuni za Kampuni ya Airtel Tanzania, Bima ya Jubilee na Kampuni ya TEHAMA ya Axieva wakisaini mikataba ya kuanzisha bidhaa mpya ya Afya Bima ambayo ni nafuu kwa wateja wa Airtel Tanzania.
Na Mwandishi Wetu - MAELEZO

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amezipongeza Kampuni ya Airtel Tanzania, Bima ya Jubilee na Kampuni ya TEHAMA ya Axieva kwa kuanzisha bidhaa mpya  ya Afya  Bima ambayo ni nafuu kwa wateja wa Airtel Tanzania.

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo  tarehe 08 Desemba, 2023 wakati alipokuwa akipewa taarifa kutoka kwa wabia hao kuhusu bidhaa hiyo kwa wateja wapatao milioni 17.5 wanaotumia mtandao wa Airtel Tanzania na kusema kuwa Serikali imetekeleza ujenzi wa miundombinu bora ya afya katika maeneo mengi nchini.

“Serikali imewekeza fedha nyingi sana kwenye kujenga miundombinu ya afya katika maeneo mengi nchini, kuna hospitali za kanda zimejengwa, vituo vya afya vingi vimejengwa, hospitali za wilaya zimejengwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.

Waziri Nape, alisema kuwa uwekezaji wa Serikali katika kutengeneza miundombinu ya afya hautakuwa na maana kama wananchi watakuwa wanapata huduma hizo kwa kusuasua na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita ikaamua kusukuma ajenda ya Bima ya afya kwa wote.

Aidha, Waziri Nape amefurahishwa na uamuzi wa Airtel Tanzania kuungana na Kampuni ya Bima ya Jubilee pamoja na kampuni ya Tehama ya Axieva kuunga mkono uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kutoa huduma za afya kwa kutumia Bima jambo ambalo ni faraja  kwa Serikali na Watanzania.

“Jambo kubwa ni kwamba Bima hii, imewalenga Watanzania hasa ambao hawana uwezo wa kuweza kujigharamia matibabu pindi wakipata shida ya kuumwa kama madereva bodaboda na Mama ntilie kwa hiyo jambo hili ni suluhisho kubwa kwao kupata huduma za afya huku Maisha yao yakiendelea”, alisema Waziri Nape.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Jubilee, Dkt. Harold Adamson amesema kuwa wamefarijika kuwapata wadau ambao wameshirikiana nao katika kuongeza thamani ya tehama na kuhudumia moja kwa moja kwenye maisha ya Watanzania.

“Sisi kama Jubilee tumefarijika kuweza kupata wadau wenzetu ili kuanzisha huduma na bidhaa hii mpya kwa Watanzania hasa wanaotumia mtandao wa airtel, bidhaa hii ya afya bima inaunga mkono juhudi za Mhe. Rais za kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na bima ya afya”, ameeleza Dkt. Adamson.

Alisema kuwa bidhaa hiyo imegawanyika katika makundi matatu ambayo ni ‘Afya Poa’ inayomuwezesha mtumiaji kuchangia shilingi 300 kwa mwezi au 3,500 kwa mwaka na kurejeshewa shilingi 20,000 kwa siku akilazwa hospitali.

Huduma nyingine ni ile ya Afya Supa ambayo mtumiaji anatakiwa kuchangia shilingi 15,000 kwa mwezi na kurejeshewa shilingi milioni 5 akiliazwa hospitali na huduma ya mwisho katika bidhaa hiyo ni Afya Dhahabu ambayo mtumiaji anatakiwa kuchangia 30,000 kwa mwezi na kurejeshewa mpaka milioni 8 akilazwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano amesema kuwa kampuni hiyo inatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya kuhakikisha watoa huduma kupitia Tehama wanatumia ujuzi huo kuwasaidia wananchi wa aina zote na kuipa thamani sekta hiyo.

Alisema kuwa Huduma na Bidhaa mpya ya Afya Bima itakwenda kwa Watanzania wapatao milioni 17.5 wanaotumia mtandao huo kuweza kupata matibabu kwa bei nafuu katika vituo zaidi ya 600 nchini na kuwawezesha wananchi kuwa na unafuu wakati wa shida ya kuumwa na kusimama kufanya kazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi