Benki ya Dunia imeendelea kuimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri na mageuzi makubwa ya kiuchumi ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipindi ambacho Dunia inahangaika na misukosuko inayotokana na athari za UVIKO 19, mizozo ya vita pamoja na kuyumba kwa soko la fedha za kigeni.
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko, walipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Jijini Marrakech, nchini Morocco.
Walisema kuwa mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisera na kisheria yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yameifanya nchi kuwa na utulivu wa kiuchumi huku wakitarajia uchumi utaendelea kuimarika zaidi baada ya Serikali kufanya maboresho makubwa ya sera mbalimbali ikiwemo ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kupitia sekta binafsi.
Pongezi hizo zinakuja siku moja baada ya Ripoti ya Mapitio ya Uchumi iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kubashiri kuwa kutokana na vigezo vyote vilivyotumika kupima mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, uchumi wa Tanzania utakua kutoka asilimia 4.7 iliyorekodiwa mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 6.1 mwaka 2024 na kuwa nchi ya pili kwa ukuaji wa uchumi katika nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, Viongozi hao waandamizi wa Benki ya Dunia, walipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi.
Akizungumza katika Mikutano hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, anayeongoza ujumbe wa Tanzania kwa niaba ya Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania. Alifafanua pia kuwa uchumi wa Tanzania unatarajia kukua kwa wastani wa zaidi ya asilimia 6.0 katika kipindi cha muda wa kati (2024 – 2026).
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia sera za kiuchumi na kifedha, ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara pamoja na kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi katika kuendesha uchumi wa nchi.
Katika kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2018 hadi kufikia mwezi Septemba 2023, Benki ya Dunia imeipatia Serikali mikopo nafuu yenye thamani ya jumla ya dola za Marekani bilioni 8.304 sawa Shilingi trilioni 20.358 ili kusaidia utekelezji wa miradi mikubwa ya maendeleo zaidi ya 28 ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa nchi na kukabiliana na hali ya umasikini katika jamii.