Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amesema kuwa, shilingi 1,600 itakuwa bei mpya ya umeme kwa uniti katika miradi midogo ya umeme iliyo nje ya Gridi ambayo itaanza kutumika tarehe 1 Agosti, 2022 ili kufanya wananchi kupata umeme wa uhakika na wawekezaji binafsi kuweza kujiendesha na kuwekeza zaidi.
Makamba amesema hayo tarehe 12 Julai 2022 akiwa katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wakati alipofika kisiwani humo kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji umeme wa uhakika.
Maamuzi hayo ya Serikali yamekuja baada ya wawekezaji binafsi wa miradi midogo ya umeme kutakiwa kuuza bei ya umeme kwa Shilingi 100 kwa uniti gharama ambayo iliwapa changamoto za kiuendeshaji na hivyo kushindwa kuwapa wananchi huduma ya umeme ya uhakika.
Akiwa kisiwani Ukara, Makamba alielezwa na wananchi wa kisiwa hicho kuwa, awali walikuwa wakilipa Shilingi 3,500 kwa uniti na walikuwa wakipata umeme kwa masaa 24 kwa siku lakini baada ya kutangazwa kwa bei ya umeme ya Shilingi 100, kampuni ya JUMEME inayotoa huduma ya umeme kisiwani humo ilianza kuwapa umeme kwa masaa sita tu kwa siku na pia kutakiwa kununua umeme kwa tokeni.
Akitoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu upangaji wa bei za nishati, alieleza kuwa unapaswa kuhusisha pande zote mbili ambazo ni Mwekezaji na Serikali hivyo, zoezi la upatikanaji wa bei mpya ya umeme limekuwa la uwazi na kwamba gharama mpya iliyotajwa haipo juu kama awali ili kutowaumiza wananchi na pia haitakuwa Shilingi 100 ili kampuni binafsi nazo ziwe na uwezo kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Sera ya Nishati imetamka wazi kuhusu bei ya nishati inayopangwa na Serikali ikiwemo umeme, gesi na mafuta kuwa lazima iendane na gharama za kuzalisha nishati husika.
Pamoja na kutangaza bei hiyo mpya, Waziri wa Nishati amezitaka kampuni husika kuhakikisha kuwa wanatoa umeme wa uhakika, wawasilishe mpango wa Biashara serikalini pamoja na kuwa na mkataba wa huduma kwa mteja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya JUMEME, Bi. Aida Kiangi aliahidi mbele ya wananchi wa UKARA kuwa kuanzia tarehe 1 Agosti, 2022 umeme kisiwani humo utatolewa kwa masaa 24.
Katika hatua nyingine, Waziri Makamba ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi 167 ambayo itasambazwa kwa Shule za Serikali za Msingi na Sekondari kisiwani Ukara pamoja na walimu wa shule hizo ili wawahamasishe wananchi wengine kutumia nishati safi.
Awali, Waziri wa Nishati alikagua vituo vidogo vya mafuta wilayani Bunda, Mkoa wa Mara katika Kijiji cha Guta B na Kibara ikiwa ni mkakati wake wa kupeleka vituo vya mafuta hadi vijijini ili wananchi wapate Nishati safi na katika mazingira salama ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetenga Shilingi bilioni 2 ili kutoa mikopo kwa wananchi wanaotaka kuwekeza katika ujenzi wa vituo hivyo vijijini.
Akiwa safarini kuelekea wilayani Ukerewe, Waziri Makamba alikagua nyaya za umeme zinazopita chini ya Ziwa Victoria ambazo zinapeleka umeme wa kiasi cha megawati 10 wilayani humo zikitokea Kisorya wilayani Bunda.