Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bashungwa Kufunga Tamasha la Muziki wa Cigogo
Jul 24, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Adeladius Makwega, (WHUSM) - Dodoma


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha kubwa la Ngoma za asili linalofahamika kama Tamasha la Cigogo litakalofanyika Julai 24 na 25, 2021 katika viwanja vya Kituo cha Sanaa Chamwino Ikulu Jijini Dodoma


Akizungumza na Vyombo vya Habari Jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Mfaume Said amesema kuwa tamasha hilo linaandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na Kituo cha Sanaa Chamwino mkoani Dodoma na litakuwa la kukata na shoka, ambapo amewasihi wakazi wa Dodoma na viunga vyake kujitokeza kwa wingi.


"Hili ni tamasha linalowakutanisha wasanii wa ngoma za asili zaidi ya 600 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania tuna imani litakuwa ni fursa kubwa kwa wapenzi wa ngoma za asili kupata burudani ambayo haijawahi kutokea", amesema Mkurugenzi huyo.


"Tunatambua na halina ubishi kuwa kwa muda mrefu Watanzania tumekuwa tukitilia mkazo Sanaa ya muziki wa dansi, muziki wa nje na bongo fleva tu lakini muziki wa kitamaduni umekuwa kando mathalani, muziki huu umekuwa haurudiwi kwa wingi na kuchezwa katika vyombo vya habari kama vile luninga na redio," alisisitiza Mfaume.


Bw. Mfaume amesema kufanyika kwa tamasha hilo la muziki wa wagogo litaibua ari ya kuikuza zaidi Sanaa ya ngoma za asili.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kituo cha Sanaa Chamwino, Dkt Kedomn Mapana amesema kuwa wao kama kituo wamekuwa wakiandaa matamasha ya namna hiyo kwa kipindi cha miaka 16 sasa na tamasha la mwaka huu litakuwa la 12 likiwa na kauli mbiu ya 'Utamaduni wetu Maendeleo yetu'.


"Tumemualika Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Deograthias Ndejembi katika ufunguzi akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas na litahitimishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mhe. Innocent Bashungwa," amesema Dkt Mapana.


Akizungumzia Tamasha hilo Mkuu wa Mtaa wa Talama Chamwino Ikulu, ndugu Andason Makolokolo amesema kuwa sasa Dodoma imekuwa jiji na kumekuwa na muingiliano wa makabila mengi lakini jumamosi na jumapili itakuwa wasaa wa Wagogo kuonyesha utamaduni wao kwa vitendo.


Kituo cha Sanaa Chamwino kwa muda mrefu kimekuwa ni miongoni mwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kwa karibu na serikali kwa kukuza sanaa na utamadauni wa Mtanzania ambapo kilisajiliwa kwa mujibu wa Sheria Nambari 23 ya mwaka 1984 ya Baraza la Sanaa la Taifa BASATA.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi