Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Barabara Ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo Kukamilika Mwaka huu
Jul 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Geita Eng. Harun Senkuku akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa ilometa 45 mkoani Geita.

Na. Mwandishi Wetu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa KM 112 inayojengwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Synohydro Corporation itakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo mkoani Kagera, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kumtaka Mkandarasi aongeze kasi ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa wakati.

“Hakikisheni mnaongeza kasi ya ujenzi ili muweze kukamilisha ujenzi huu kwa wakati haraka iwezekanavyo”, amesema Prof. Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd anayejenga barabara ya Uyovu-Bwanga kilometa 45 kwa kiwango cha lami mkoani Geita.

Amemsisitiza Mkandarasi kuzingatia viwango vilivyopo katika mkataba kwani mwisho wa siku lazima watanzania wapate barabara inayokidhi mahitaji yao na ubora wake.

Amewapongeza wasimamizi wa barabara hiyo ambao ni kutoka kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kupitia kitengo chake maalum cha wahandisi washauri wazawa (TECU), kwa kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi M/S Sinohydro Corporation kwa ukaribu.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Geita Mhandisi. Harun Senkuku amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa changamoto ya fidia iliyokuwa inawakabili sasa imemalizika na kiasi cha shilingi milioni 700 zimetumika kukamilisha ulipaji fidia kwa wakazi wote.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67 mkoani Geita.

Mhandisi Senkuku amemhakikishia Waziri kuwa TANROADS itaendelea kumsimamia Mkandarasi huyo ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha ya Serikali inapatikana.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo kilometa 112 umehusisha ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilometa 45 na barabara ya Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi