Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Barabara ya Njombe - Makete Kufungua Fursa za Utalii, Neema kwa Wananchi
Aug 10, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika - MAELEZO, Makete

Barabara ya Njombe - Maronga - Makete yenye urefu wa kilomita 107.4 ambayo thamani ya ujenzi wake ni Shilingi bilioni 243.4 inatajwa kufungua fursa za uchumi na utalii wa mkoa wa Njombe.

"Barabara hii itasaidia kufungua utalii pamoja na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, ombi langu kwenu ni kuilinda kwa vile kumekuwa na tabia ya watu kuchimba michanga kwenye barabara" Amesisitiza Rais Samia.

Akizungumza leo wilayani Makete mara baada ya kuzindua barabara hiyo, Rais Samia ameeleza namna ambavyo mkoa huo utanufaika na kukuza uchumi wake.

Rais Samia ameongeza kuwa Wilaya hiyo ya Makete itabadilika na hivyo wategemee wageni wengi watakaotembelea na kuwekeza.

Aidha, Afisa Tarafa wa Matamba, Bw. Bujo Mwakatobe ameeleza kuwa awali wananchi wa Makete walisafiri kwa tabu kwenda maeneo mbalimbali na kutopata huduma muhimu kwa wakati.

"Tulikuwa na basi moja tu linalosafiri kutoka Iringa, Mafinga, Makambako na Njombe kuleta abiria Ikonda na Makete na hakukuwa na usafiri mwingine. Pia, wakati wa masika tulikwama sana njiani hasa katika milima ya Mang'oto kwa sababu ya utelezi" Amesema Mwakatobe.

Ameongeza "Baada ya barabara sasa magari ya kuelekea maeneo mbalimbali yameongezeka, mfano kuna mabasi yanayokwenda Dar Es salaam na Mbeya kila siku, uwekezaji wa hoteli za kisasa umeanza, pia watalii wameanza kuja kwenye Hifadhi ya Kitulo kwa vile barabara inapitika wakati wote".

Naye, Mjasiriamali, Bi. Anunize Sanga ameeleza kuwa baada ya barabara hiyo sasa wanatumia saa chache kufika Njombe na usafirishaji wa bidhaa umekuwa rahisi.

"Tulipokuwa tukienda kutibiwa hospitali ya Ikonda tulifika kwa tabu sana na wengine walikuwa wanafia njiani lakini sasa ni tofauti mgonjwa anawahi kufika kwa hivyo tunapona kupitia barabara hii" Amesisitiza Bi. Sanga

Vilevile, barabara hiyo imerahisisha usafirishaji wa zao la parachichi kutoka Njombe kwenda maeneo mengine ikiwemo nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi