Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Barabara ya Mbeya - Chunya – Makongolosi – Singida Kuifungua Tanzania
Aug 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Chunya katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja Matundasi wilayani humo mkoani Mbeya tarehe 06 Agosti, 2022.

Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Mbeya

Barabara ya  Chunya - Makongolosi ambayo imezinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Mbeya  ni sehemu ya barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Singida  yenye kilomita 528 ambayo ikikamilika itaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Tabora na Singida ambapo pia itaunganisha nchi za kusini na mashariki mwa Tanzania na kufungua fursa zaidi za kiuchumi.

Akizungumza leo, Chunya mkoani Mbeya mara baada ya kuzindua barabara hiyo kipande cha Chunya – Makongolosi Rais Samia amesema kuwa lengo la Serikali la kujenga barabara hiyo ni kuifungua Tanzania na kuongeza fursa za usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

“Furaha yangu na faraja yangu leo ni kuona wananchi wa Matundas na Chunya kwa ujumla wananufaika na fursa ya barabara hii ambayo ikikamilika ujenzi wake kwa upande wa kusini itaiunganisha Mbeya hadi mpakani Tunduma na nchi jirani ya Zambia, mikoa ya Mbeya, Singida na Tabora pamoja na nchi za mashariki mwa Tanzania, sio tu barabara hii bali mtanufaika pia na umeme na maji masuala ambayo tunaendelea kuyafanyiakazi” Amesisitiza Rais Samia 

Aidha, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Mbeya kwani itasaidia kuimarisha shughuli za kilimo na biashara na hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi