Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Barabara Hii ni Miujiza Kwetu - Ngayamagulu
Aug 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika - MAELEZO, Mufindi

Wananchi wa Mkonge wilayani Mufindi mkoani Iringa wamefurahishwa na uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Sawala - Iyegea - Lulanga yenye urefu wa kilomita 40.7 ambayo inatajwa kurahisisha usafirishaji wa zao la chai, mbao na mazao mengine kwenda katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza leo wilayani hapo katika mahojiano maalum na Afisa Habari wa Idara ya Habari - MAELEZO, Msafirishaji wa Mazao, Bw. Stephan Ngayamagulu ameeleza kuwa kabla ya barabara hiyo usafirishaji wa mazao ulikuwa mgumu na wa gharama kubwa kwa wakulima.

"Tangu nimezaliwa hadi sasa hivi nina miaka 61 sijawahi kuona barabara nzuri kama hii huku kwetu, hapo awali umbali wa kilomita 25 tulitumia wiki moja au mbili kusafiri, tunamshukuru sana Rais Samia kwetu hii ni miujiza kwa vile sasa tunasafirisha chai na mazao mengine kwa wakati" Ameeleza Ngayamagulu.

Ameongeza kuwa kabla ya barabara hiyo wakulima wenye magari pekee ndio waliweza kusafirisha chai kutoka shambani hadi viwandani na wengine walishindwa.

Aidha, Mkulima, Bi. Devota Nyunza ameeleza kuwa changamoto ya barabara ilihatarisha pia usalama wao na mazao yao.

"Usafiri ulikuwa mgumu sana almanusura tupoteze uhai kwa ajali kwa sababu ya ubovu wa barabara sasa tunamshukuru sana Rais Samia. Pia, najua baada ya barabara hii nitauza mazao yangu kwa bei nzuri na usafiri ni gharama nafuu namshukuru Rais Samia kwa kutujali wananchi wa Mufindi.

Naye, Feni Msindila ameeleza kuwa barabara hiyo imerahisisha gharama za usafiri ambapo awali nauli ya basi kutoka Mkonge hadi Sewala ilikuwa shilingi 5,000/= na sasa ni 2,000/=.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seif ameeleza kuwa Rais Samia ameweka jiwe la msingi katika barabara hiyo ya Sawala-Iyegea - Lulanga yenye urefu wa kilomita 40.7 ambapo kati ya hizo kilomita 30.3 tayari ujenzi wake umeshakamilika na kilomita 10.7 ziko kwenye hatua za usanifu na ujenzi wake utaanza mwaka 2023/24.

Mhandisi Seif amefafanua "Sehemu hiyo ya kilomita 30.3 imejengwa kwa fedha za ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya kupitia pragramu inayoratibiwa na Wizara ya Kilimo na kilomita 10. 7 zitajengwa na fedha za Serikali".

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika barabara hiyo wakati akiwa katika ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi