Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Baadhi ya Taasisi za Umma Hazizingatii Miongozo ya Matumizi ya Fedha - CAG
Apr 06, 2020
Na Msemaji Mkuu

Adelina Johnbosco - MAELEZO

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), CPA. Charles Kichere amesema kuwa matumizi ya fedha kwa taasisi za ummma na Serikali Kuu hayazingatii mapendekezo na taratibu za miongozo iliyowekwa katika matumizi ya fedha.

Amebainisha hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya ukaguzi aliyowasilisha bungeni leo Aprili 6, 2020 kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30, Juni, 2019 ambayo ni ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, Miradi ya maendeleo na vyama vya siasa.

‘’Kati ya mapendekezo 266 yaliyotolewa miaka iliyopita, mapendekezo 82 ambayo ni asilimia 31 pekee yalitekelezwa kikamilifu, mapendekezo 95 asilimia 36 utekelezaji wake unaendelea, na mapendekezo 67 sawa na aslimia 25 utekelezaji wake haujaanza hadi sasa huku mapendekezo 22 sawa na asilimia 8 yamepitwa na wakati ,‘’ amebainisha Kichere

Hata hivyo, amesema ikilinganishwa na mwaka mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30, Juni, 2018, kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Ofisi yake kimeongezeka ambapo kati ya mapendekezo 350 yaliyotolewa miaka iliyopita, mapendekezo 80 sawa na asilimia 22.9 yalitekelezwa kikamilifu.

Vilevile amebainisha ongezeko la makusanyo ya fedha chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mwaka unaoishia  Juni 30, 2019 kuwa ni kiasi cha Shilingi trilioni 15.74 ambapo mwaka uliopita 2017/2018 makusanyo yalikuwa trilioni 15.40 hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.

Katika hatua nyingine CAG Kichere amebainisha kuwa deni la Serikali ni himilivu licha ya kuwepo ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka uliopita ulioishia tarehe 30, Juni. 2018

‘’Hadi sasa deni la Serikali ni Shilingi  trilioni 53.11 ambapo deni la ndani ni Sh. trilioni 14.86 huku deni lanje ni Sh. trilioni 38.24 ikiwa ni ongezeko la Shilingi trillion 2.18’’.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Hesabu za Serikali, Naghenjwa Kaboyoka, amesema wataziripoti taasisi za umma na Serikali Kuu kwa Rais kwa kubainika kuwahamisha vituo vya kazi wakaguzi wa ndani wa ofisi hizo baada ya kuweka hadharani matumizi mabaya ya fedha katika ofisi hizo.

‘’Tunazo rekodi za ofisi zilizowahamisha wakaguzi wao wa ndani kama adhabu ya kutoa taarifa za matumizi mabaya ya fedha na kuwaajiri wakaguzi wapya huku wakiwapa vitisho ili kuwa kimya pindi wabainipo matumizi mabaya ya fedha katika ofisi husika,’’ alisisitiza Kaboyoka

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi