Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ametoa wiki moja kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kukamilisha taratibu za ndani na kumlipa Mkandarasi wa Kampuni Estim Construction anayejenga barabara ya kiwango cha zege (km 15), kutoka Kwala hadi Vigwaza ili ikamilike kwa wakati.
Naibu Waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani na kushuhudia uchelewaji wa ujenzi wa barabara hiyo kutokana na malipo.
“Urasimu wa kutoa fedha ni miongoni mwa sababu za kuchelewa kwa mradi huu hivyo nawapa siku saba kamilisheni taratibu zote zinazotakiwa na mumlipe mkandarasi huyu na Serikali inatarajia kupokea barabara hii mwishoni mwa mwaka”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Ameitaka TPA kuhakikisha wanakamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa kumaliza eneo la Bandari Kavu kwani limechukua muda mrefu hali inayosababisha upungufu wa ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam na kutofikiwa kwa lengo la kupunguza msongamano.
Kwa upande wake Meneja Miliki wa TPA, Bw, Alexander Ndibalema amemhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa maelekezo yake yatafanyiwa kazi kwa haraka.
Meneja Ndibalema amesema TPA imeshaunda kamati ya kupitia zabuni zilizoombwa na ndani ya muda mfupi zoezi hilo litahitimishwa na mradi huo kuendelea kutekelezwa.
Naye Mhandisi Mkazi wa mradi huo kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Jacob Mambo, amemhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 60 na asilimia zilizobaki zitakamilika ndani ya miezi mitatu.
Mradi wa ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 80 ambazo zinahusisha ujenzi wa Barabara ya kutoka Kwala hadi Ruvu KM 15.5, uendelezaji wa eneo la hekta 5, reli kilomita 1.3 na ujenzi wa uzio wa eneo hilo.