Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Asilimia 95 ya Wananchi Kufikiwa na Huduma ya Maji Safi Ifikapo 2020.
Feb 27, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

Serikali imesema kuwa ifikapo mwaka 2020 itahakikisha asilimia 95 ya wakazi wote wanapata huduma ya majisafi mijini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ujenzi wa Viwanda hapa nchini.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya majisafi na majitaka inayotekelezwa na kusimamiwa na Serikali katika Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso amesema kuwa  Wizara yake itahakikisha kuwa lengo la kuwafikisahia wananchi wote huduma ya maji linafikiwa kwa wakati.

"Kama kuna madai yoyote ya wakandarasi na mna uhakika kuwa kazi imefanyika kwa mujibu wa mkataba yaleteni Wizarani nasi hatutakawia kuyalipa"  Alisisitiza Mhe. Aweso

Akifafanua Mhe Aweso alisema  kuwa Wizara ya Maji kamwe haiwezi kuwa kikwazo cha utekelezaji wa miradi ya maji hivyo imejipanga vyema kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Katika ziara hiyo Mhe. Aweso alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo na kupata taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji wilayani humo ambapo ilielezwa kuwa imeimarika hasa baada ya mitambo ya maji ya ruvu juu na ruvu chini kukamilika.

Aidha alitembelea miradi ya maji ya Hondogo na King'azi inayotekelezwa na Manispaa, tenki la maji la Kibamba ambalo lilijengwa na DAWASA na mradi wa majitaka wa Mburahati shuleni  unaojengwa chini ya ufadhili wa Asasi ya BORDA kwa kushirikiana na Manispaa.

Moja ya changamoto inayokabili sekta hiyo ni tatizo la uvujaji wa maji ambapo Mhe. Aweso alilitaka shirika la majisafi na majitaka Dar es salaam DAWASCO kuongeza jitihada za kudhibiti tatizo la upotevu wa maji kutoka katika miundo mbinu yakusafirishia maji kwa kushirikisha wananchi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi