Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Asilimia 80 ya Madini ya Tanzanite Husafirishwa Nje ya Nchi kwa Magendo.
Sep 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_12388" align="aligncenter" width="768"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017. Katikati ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.[/caption]

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma. Asilimia 80 ya Madini ya Tanzanite yanayochimbwa nchini hutoroshwa nje ya nchi kwa njia ya magendo na asilimia 20 tu ndiyo inayoingizwa katika mfumo wa kodi. Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite Mhe. Dotto Mashaka wakati wa uwasilishwaji wa taarifa hiyo leo, katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma. “Biashara ya Tanzanite imegubikwa na wizi mkubwa ambapo takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1998 ni kilo 13.2 tu za Tanzanite zimezalishwa nchini, sawa na kuzalisha gramu 700 za Tanzanite kwa mwaka kwa kipindi chote cha miaka 19,” amefafanua Mhe. Biteko.

Biteko amesema kuwa Kamati yake imebaini vichochoro 400 vinavyotumika kutorosha Tanzanite nchi jirani na kuikosesha Tanzania mapato yanayotokana na madini hayo yanayotoroshwa kinyemela.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Kuchunguza Biashara ya Almasi Mhe. Musssa Azzan Zungu amesema kuwa madini ya Almasi yamekuwa yakisafirishwa nje ya nchi kama malighafi ambapo huko husafishwa na kukatwa vizuri na baadae kuuzwa kwa gharama kubwa.

Usafirishwaji wa madini hayo kama malighafi Tanzania imepoteza fedha nyingi ambapo kwa nchi ya Botswana inauza Almasi yake ndani ya nchi kwa Dola 1900 na Tanzania tunauza nje ya nchi kwa Dola 300.

Vile vile Mhe. Zungu amesema kumekuwepo a udangabyifu mkubwa katika usafirishaji wa madini ya Almasi nje ya nchi ambapo Kamati yake imegundua kuwa kuna Almasi ilithaminishwa hapa nchini ambayo ilikuwa na thamani ya Dola Milioni 15 lakini iliuzwa Dola Milioni 10 nje ya nchi.

Aidha, Kamati zote hizo zimeishauri Serikali kupitia upya mikataba ya madini ambayo Serikali imeingia na makampuni ya madini yanayoisababishia Serikali hasara kubwa. Vile vile wameshauri Serikali kuleta wawekezaji watakaoleta mitambo ya kuchuja madini ambayo itaongeza thamani ya madini na kuuzwa kwa gharama ya juu.

Nae, Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amesema kuwa Watanzania waungane katika kutetea maslahi ya nchi hasa katika masuala ya madini. akitolea mfano Mhe. Ndugai alisema “Zipo koo ambazo zinatofautiana lakini kuna kipindi ambacho huungana katika kutetea maslahi ya koo zao”.

Aidha, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa zaidi ya makampuni 10 yamejitokeza kujenga mitambo ya kuchujia madini nchini, Hivyo madini yote yatakuwa yakichenjuliwa hapa nchini mara mitambo hiyo itakapoanza kufanya kazi.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa ushauri wote uliotolewa na kamati zote mbili utafanyiwa kazi kwa muda muafaka tena kwa kipindi kifupi.

Kamati maalum za kuchunguza biashara ya Tanzanite na Almasi ziliundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapema Juni mwaka huu, baada ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupokea taarifa ya kamati ya pili ya kuchunguza mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia) na kulitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano nao kufanya kitu juu ya madini yanayosafirishwa nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi