Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

APRA Kuitangaza Afrika na Fursa Nyingi za Kiuchumi - Msigwa
May 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mawazo Kibamba, MAELEZO.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa amesema Mkutano wa 33 wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Umma Barani Afrika (APRA) utakaoanza Mei 24, umekuja kwa wakati muafaka wakati Tanzania ikifanya kila jitihada za kutangaza fursa za Kiuchumi ikiwepo Utalii na Uwekezaji.

Amesema Tanzania na Afrika kwa ujumla ni nchi zinazofanya maendeleo makubwa kwa kuimarisha huduma na miundombinu mambo ambayo ukienda kwenye nchi zingine za nje ya Bara la Afrika ni kama hayafahamiki sana ambapo sasa mkutano huo pamoja na kujadili namna ya kuzinadi nchi zao, pia unalenga kuitangaza Afrika na fursa zake.

“Huu ni mkutano wa 33 wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Umma Barani Afrika, kwa mara ya kwanza unafanyika Tanzania, ni mkutano muhimu sana katika safari ya kuitangaza nchi yetu vizuri, Maafisa Uhusiano watajadili namna ya kuinadi Afrika duniani, kama unavyofahamu kumekuwa na juhudi mbalimbali zinazofanyika katika mataifa mbalimbali huko duniani yakieleza katika Vyombo vya Habari vya kimataifa habari mbaya kuhusu Afrika kwamba kuna njaa, hakuna miundombinu, hakuna shughuli za kiuchumi, lakini sasa hapa Maafisa Uhusiano tangu mwaka 1975 walipofanya uamuzi wa kuanzisha chama hiki wakaona kwamba kuna haja ya sisi wenyewe Waafrika kuieleza Afrika, kuyaeleza mazuri ya Afrika”, amesema Msigwa.

Amesema Afrika ina rasilimali nyingi lakini uwekezaji haujafanyika vya kutosha na kutokana na rasilimali hizo kutotumika ipasavyo tumejikuta tuna matatizo ambayo yangeweza kutatuliwa kama uwekezaji wa kutosha ungefanyika Afrika

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Umma Barani Afrika, Bw. Yomi Badejo-Okusanya amesema mkutano huo pamoja na kujadili ushirikiano wa pamoja wa kuzitangaza fursa za kiuchumi kwenye nchi za Afrika, pia unalenga kuimarisha mkakati wa mawasiliano kwenye Taasisi na Mamlaka ya Umma.

“Tuna furaha kuwa hapa Tanzania kwa ajili ya kushiriki mkutano wa 33 wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Umma Barani Afrika, mada kuu ya mkutano huu ni Afrika Imara yenye uwezo wa kuhimili vishindo vya masuala ya uhusiano kwenye medani za kimataifa, lengo letu ni kuitangaza Afrika, kuzitangaza nchi zetu na fursa za kiuchumi” amesema Bw. Yomi Badejo-Okusanya.

Nae Rais wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Umma wa nchini Tanzania Bw. Assah Mwambene amesema mkutano huo ni muhimu sana katika Afrika kwa sababu hakuna jambo jema ambalo lilikuwa likiandikwa kuhusu nchi hizo ambapo sasa umefika wakati wa kuwa na sauti ya kujisemea wenyewe.

“Mara nyingi tumetumia midomo na sauti za Vyombo vya Habari vya kimataifa katika kusema yale yote mazuri yanayotokana na Afrika, kwa sasa tunahisi ni wakati muafaka kwamba Afrika iamke na iwe na wasemaji wake wenyewe na kueleza ukweli ambao umekuwa ukipindishwa kwa miaka mingi kutokana na uoga wetu” amesema Mwambene.

Mwisho.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi