Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Ashiriki Majadiliano na Viongozi Wakuu wa Afrika Uswisi
May 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango amesema eneo huru la kibiashara barani Afrika ni fursa kubwa kwa nchi za bara hilo katika kukuza uchumi namaendeleo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa majadiliano maalum ya viongozi wakuu wa nchi za Afrika yalioshirikisha wadau na marafiki wa nchi za Afrika kutoka mataifa mengine, majadiliano yaliyofanyika katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi duniani unaoendelea Davos nchini Uswisi.

Amesema katika kutumia fursa hizo nchi za Afrika zinapaswa kupunguza vikwazo mbalimbali ikiwemo vya kikodi katika ufanyaji biashara pamoja na kuimarisha miundombinu itakayorahisisha biashara hizo katika eneo hilo huru.

Ameongeza kwamba ni muhimu kuwekeza katika teknolojia itakayorahisisha kufanya biashara na malipo mbalimbali pamoja na kufanya ubia na sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na mataifa mengine ili kuongeza uzalishaji katika viwanda.

Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea kuhakikisha wananchi wanaelewa fursa zilizopo katika eneo huru la biashara barani Afrika pamoja na kuimarisha sekta ya uwekezaji kwa kuingia ubia nawadau mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika ilikuweza kufanya biashara katika ukanda huo huru kwa tija zaidi.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameshiriki katika mjadala uliohusu ufufuaji uchumi pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kurejesha amani na mtangamano duniani ambapo viongozi hao wamejadili namna ya kushirikiana katika kukabiliana kutatua matatizo ya kisiasa yanayopelekea vita na migogoro. 

Aidha Makamu wa Rais amesema ni muhimu dunia inapokabiliana na changamoto kama vita kutosahau changamoto zingine ikiwemo upungufu wa chakula pamoja na kuhakikisha Afrika inashirikishwa katika maamuzi mbalimbali ya dunia. Amesema Afrika ina fursa kubwa ya kuchangia katika kuleta amani na suluhisho la upatikanaji wa chakula kama itaungana na mataifa mengine kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Makamu wa Rais yupo Davos nchini Uswisi kumwakilisha Rais wa Jamhuri yaMuungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi duniani unaoshirikisha wakuu wa nchi, wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa pamoja na wafanyabiashara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi