[caption id="attachment_5920" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohamed Janabi akiteta jambo na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi yake alipotembelea Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam leo. Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo Bi. Anna Nkinda.[/caption]
Na: Frank Mvungi
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao hasa magonjwa ya moyo katika msimu huu wa maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara ya Dar es Salaam yanayofanyika katika viwanja vya JK Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika viwanja vya maonesho hayo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi amesema kumekuwa na muitikio mkubwa sana kwa wananchi kutembelea banda lao ambapo amesema kuwa kwa siku takribani watu 700 wanafika katika banda hilo kwa ajili ya kupata huduma na ushauri.
[caption id="attachment_5923" align="aligncenter" width="750"]“Ni vizuri watanzania wakatumia fursa hii kufika hapa na watapatiwa baadhi ya vipimo na ushauri bure katika banda letu lililopo ndani ya viwanja vya sabasaba kwa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi wake kwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma zote za msingi zenye kiwango na ubora,” Alisisitiza Prof. Janabi
Akifafanua Prof. Janabi amesema Taasisi hiyo imedhamiria kuwahudumia wananchi wakati wote wa maonesho na hata baada ya hapo wapo tayari kuwahudumia wale wanaohitaji huduma katika taasisi hiyo.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imekuwa ikitoa huduma za upasuaji wa moyo tangu kuanzishwa kwake hali inayosaidia kupunguza gharama zilizokuwa zinatumika kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu kwa kipindi kirefu sasa.