Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

4R za Rais Samia Zakuza Sekta ya Utamaduni na Sanaa
Feb 28, 2025
4R za Rais Samia Zakuza Sekta ya Utamaduni na Sanaa
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Bi. Nyakaho Mahemba, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita leo tarehe 28 Februari, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Falsafa ya 4R inayojumuisha Ustahimilivu, Maridhiano, Mageuzi na Ujenzi mpya iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mwelekeo wa kipekee katika kukuza sekta ya utamaduni na sanaa ambapo falsafa hiyo imetumika kama nyenzo muhimu katika ujenzi wa sekta imara na endelevu.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Bi. Nyakaho Mahemba ameyasema hayo leo Februari 28, 2025 jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko huo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa Waandishi wa Habari ikiwa ni programu iliyoandaliwa na Idara hiyo.

“Falsafa ya 4R kwa ujumla ndiyo imewezesha Wasanii kupata mikopo kwa masharti rahisi na kuanzisha au kukuza miradi ya sanaa hivyo kuongeza uwezo wao wa kurejesha mikopo kwa ufanisi, mikopo inayotolewa itakuwa endelevu ili wasanii waweze kufanikiwa katika kipindi kirefu, Serikali imejizatiti kutoa rasilimali za kifedha na vifaa muhimu kwa wasanii pamoja na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, wasanii na wadau wa sekta ya utamaduni”, amesema Bi. Nyakaho.

Bi. Nyakaho ameeleza kuwa kupitia Maridhiano, Serikali inafanya kazi kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa sekta ya sanaa inaboresha fursa kwa wasanii ambapo Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umetoa mikopo iliyowezesha wasanii kupata nafasi ya kuonesha vipaji vyao, kuhakikisha kuwa wanapata mapato na kuendelea kukuza sanaa katika mazingira bora.

Vile vile, Serikali kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa imekuwa mstari wa mbele katika kuwekeza katika mafunzo na elimu ya wasanii ili kuwawezesha kuboresha ujuzi wao na kuongeza ustahimilivu wao katika kukabiliana na changamoto za kimataifa. Falsafa ya ustahimilivu pia umehusisha ushirikiano wa karibu kati ya wasanii, serikali, na wadau wa sekta binafsi.

Katika sekta ya utamaduni na sanaa, falsafa ya mageuzi inaendelea kufanyika, hususan katika kuboresha miundombinu ya kazi ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa imejizatiti kutoa mikopo ili kuboresha majumba ya sanaa, vituo vya maonesho na kuanzisha maeneo ya kazi bora ambayo yatatoa nafasi kwa wasanii kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa ubora.

Katika falsafa ya ujenzi mpya, Rais Samia ameanzisha mikakati ya kisasa ya usambazaji wa kazi za sanaa, kama vile muziki, filamu, na uchoraji, kwa kutoa mikopo inayowawezesha wasanii kufikia masoko ya kimataifa ikijumuisha kumudu gharama za matumizi ya teknolojia mpya katika utengenezaji na usambazaji wa kazi za sanaa.

Bi. Nyakaho amemalizia kwa kutoa pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri, uliojaa mafanikio mengi makubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita ambao umejenga mazingira mazuri, bora, wezeshi na rafiki ya kusimamia sekta ya Utamaduni na Sanaa kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi