Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TRA Yafafanua Mabadiliko ya Sheria Kwenye Viwango vya Kodi
Nov 14, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_48849" align="aligncenter" width="750"] Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Emmanuel Msambwa (kulia) akimuelimisha Mfanyabiashara wa duka la nguo wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi Wilayani hapo.[/caption]

Na: Veronica Kazimoto -Mvomero

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi wa mabadiliko ya viwango vya kodi kama vilivyoainishwa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 ambapo mabadiliko hayo yamegusa Sheria za Kodi ya Mapato, Ongezeko la Thamani (VAT), Usajili wa Vyombo vya Moto pamoja na Usalama Barabarani.

Akizungumza wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani Morogoro katika Wilaya ya Mvomero, Afisa Msimamizi wa Kodi Mkuu wa TRA, Julius Mjenga amesema kuwa, mabadiliko katika sheria ya kodi ya mapato, jedwali la viwango vya kodi kwa wafanyabiashara wadogo wakazi, vimepunguzwa kutoka sh. 150,000 hadi kufikia sh. 100,000, kwa wale wenye mzunguko wa mauzo yanayozidi sh. milioni nne hadi milioni 7 kwa mwaka.

“Kwa wafanyabiashara wenye mauzo kati ya sh. milioni saba hadi sh. milioni 11, viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia sh. 250,000 kutoka sh. 318,000 iliyokuwepo hapo awali,” alisema Mjenga.

[caption id="attachment_48850" align="aligncenter" width="750"] Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Ernesta Shirima (kushoto) akiwaelimisha Vijana wa Bodaboda wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kuhusu umuhimu wa kuhamisha kadi za vyombo vya moto wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi Wilayani hapo.[/caption] [caption id="attachment_48851" align="aligncenter" width="750"] Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rahabu Kibona (kulia) akichukua maelezo ya Mlipakodi kwa ajili ya maandalizi ya kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi Wilayani hapo.(Picha zote na TRA)[/caption]

Pia, kwa wafanyabiashara wenye mauzo kati ya sh. milioni 11 hadi sh. milioni 14, viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia sh. 450,000 kutoka sh. 546,000.

“Lengo la kupunguza viwango hivi ni kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari na kuongeza Mapato ya Serikali,” alifafanua Mjenga.

Kwa upande wa sheria ya usajili na uhamishaji wa umiliki wa vyombo ya moto, Mjenga ameeleza kuwa, ada ya kupata nakala ya kadi ya gari ni sh. 50,000, pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) sh.30,000 na pikipiki ni sh. 20,000 badala ya sh. 10,000 iliyokuwa ikitozwa kwa vyombo vya aina hiyo kabla ya tarehe 1 Julai, 2019.

Aidha, akizungumzia juu ya mabadiliko ya viwango vya leseni za udereva chini ya sheria ya usalama barabarani, Mjenga amesema kuwa, leseni ya udereva inalipiwa sh. 70,000 kila baada ya miaka mitano ambapo kabla ya mabadiliko ilikuwa inalipiwa sh. 40,000 kila baada ya miaka mitatu.

“Mabadiliko haya kwa ujumla wake yamelenga kuongeza fursa kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla kuongeza ufanisi katika biashara zao na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. Hivyo, natoa rai kwa walipakodi wote kutumia fursa hii adhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alieleza Mjenga.

Wiki ya elimu kwa mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019 ambapo shughuli zinazofanyika ni pamoja na usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), kupokea mrejesho, kusikiliza kero na kujibu maswali yanayoulizwa na wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi