[caption id="attachment_34720" align="aligncenter" width="750"] Mfano wa Meli mpya itakayojengwa ambayo Mkataba wake umesainiwa. Meli hiyo itakuwa na Urefu wa Mita 90, Kimo mita 10, uwezo wa kubeba abiria 1200 magari madogo 20, mizigo tani 400 na itakuwa ikisafiri kwa muda wa masaa sita tu kutoka Mwanza mpaka mkoa wa Kagera.[/caption]
Na: Fatma Salum-MAELEZO, Dar es Salaam.
Serikali imesaini mikataba minne ya miradi ya uundwaji wa meli mpya, chelezo na ukarabati wa meli mbili chakavu yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 152.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo iliyofanyika leo mkoani Mwanza, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa miradi hiyo yote itatekelezwa katika bandari ya Ziwa Victoria mkoani humo.
“Nimefurahishwa sana na hatua hii ya utiaji saini wa ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizokuwepo, dhumuni ni kuboresha huduma ya usafiri katika Ziwa Victoria,” alisema Rais Magufuli.
Pia alibainisha kuwa fedha zote za utekelezaji wa miradi hiyo ni fedha za Serikali ya Tanzania zilizopatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya kodi hapa nchini.
“Fedha hizi zote ni zetu, Wakorea ni wakandarasi tu,nawaomba Watanzania msikwepe kodi na muamini kuwa fedha mnazozikusanya hazitapotea, tutazisimamia,” alisisitiza Rais Magufuli.
Aidha katika hafla hiyo Rais Magufuli aliahidi kutoa shilingi bilioni 3.7 ndani ya wiki mbili kwa ajili ya kulipa madeni ya mishahara ya wafanyakazi wa Kampuni ya Huduma za Meli.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Erick Hamisi alibainisha kuwa ujenzi wa meli hiyo ya kisasa katika Ziwa Victoria utagharimu shilingi bilioni 88.76 na itakuwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mizigo, abiria 1200 na magari madogo 20.
“Meli hii itakuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Maziwa Makuu, itakuwa na urefu wa mita 90 na kimo cha mita 10.9 sawa na ghorofa 3 kwenda juu,” alisema Hamisi.
Pia alieleza kuwa ujenzi wa meli hiyo utakamilika katika kipindi cha miezi 24 na itajengwa katika bandari ya Mwanza na mradi huo utatoa ajira kwa watanzania zaidi ya 250.
Aidha Hamisi alisema kuwa miradi mingine ni ujenzi wa chelezo (slipway) itakayotumika kujenga meli mpya katika Ziwa Victoria ambayo itagharimu shilingi bilioni 35.99 na ikikamilika itaweza kubeba meli yenye uzito wa tani 4000 na itatumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa meli mbalimbali.
“Pia tumesaini mikataba ya ukarabati mkubwa wa meli 2 za Mv Butiama na Mv Victoria ambao utagharimu shilingi bilioni 27.61,” alisema Hamisi.
Pia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni juhudi za Rais John Magufuli katika kuhakikisha anasimamia vyema makusanyo ya fedha za watanzania.
Naye Balozi Wa Korea Kusini nchini Tanzania, Song Geum Yong alisema kuwa anawapongeza wahusika wote kwa kusaini mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa meli mpya na chelezo.
“Maendeleo haya yote yanatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na watanzania wakiongozwa na Rais Dkt. John Magufuli,” alisema Yong.
Miradi yote hiyo itajengwa na wakandarasi kutoka Korea Kusini wakishirikiana na baadhi ya wakandarasi kutoka Tanzania.