Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kliniki ya Biashara Kuwakomboa Wafanyabishara
Jul 03, 2018
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage (katikati) akizindua Kliniki ya Biashara katika Maonesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam leo, lengo la Kliniki hiyo ni kutatua changamoto mbalimbali za biashara na wafanyabiashara.

Na Fatma Salum
Serikali kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania  (TanTrade) imeanzisha Kliniki ya Biashara itakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiashara wakiwemo wajasiriamali wadogo.
Kliniki hiyo imezinduliwa leo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mwijage alisema kuwa Kliniki hiyo itakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara nchini wakiwemo wajasiriamali wadogo kwa kuwa itawawezesha kutatua changamoto zao kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa ili waweze kukuza biashara zao na uchumi wa taifa kwa ujumla.
"Taasisi zote za Serikali zinazohusika na biashara zihakikishe wafanyabiashara wanasaidiwa kutatua changamoto kwa haraka bila ya urasimu kupitia kliniki hiyo na zishirikiane katika kuwasaidia wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao vizuri bila vikwazo vyovyote visivyo na msingi," alisema Mwijage.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) alisema kuwa mamlaka hiyo imejipanga vizuri kutoa huduma kupitia kliniki hiyo ambayo makao makuu yake yatakuwa Jijini Dar es Salaam na kutakuwa na ofisi katika kila mkoa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Zanzibar, Hassan Hafidh aliwataka watanzania kutumia vizuri fursa za biashara zilizopo na waendelee kutengeneza bidhaa zenye ubora ambazo zitaweza kuuzwa kwenye soko la ndani na nje ya nchi.
Kliniki ya Biashara itajumuisha Taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya biashara ikiwemo usajili, kodi, mazingira, afya, viwango na kadhalika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi