Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Dkt Kalemani Afanya Mazungumzo na Waziri wa Mafuta wa DRC

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiwa na Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa Aime Ngoi-Mukena (kulia) na Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini DRC, Michael Sereki.

Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amekutana na Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa  Aime Ngoi-Mukena ambapo wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa siku za nyuma ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ya Waziri wa Nishati, jijini Dar es Salaam na yalijikita katika kujadili sehemu kuu nne za ushirikiano ambazo ni kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa Tanganyika, usafirishaji mafuta safi kutoka bandari ya Tanga na Dar Es Salaam na utumiaji wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) kwa ajili ya mafuta kutoka DRC katika Ziwa Albert.

Eneo jingine walilojadili ni ushirikiano wa wataalam wa Sekta ya Mafuta na Gesi wa nchi hizo mbili ili kuongeza uelewa na kupata uzoefu wa kazi.

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa Aime Ngoi-Mukena (kushoto) akizungumza na wataalam wa miundombinu ya bomba la Tazama alipotembelea kuangalia uendeshaji wa Bomba hilo.

Waziri wa Nishati wa DRC, alitumia fursa hiyo kuomba msaada wa watalaam wa gesi wa Tanzania  kwenda kufundisha vijana nchini DRC baada ya nchi hiyo kufungua Chuo Kikuu cha Mafuta na Gesi.

Kwa upande wake, Dkt Kalemani alimweleza Waziri huyo wa DRC kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kujali ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na DRC na hivyo Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande  mbili yanatakelezwa na kuleta manufaa kwa wananchi wa Tanzania na DRC.

Kwa pamoja Mawaziri hao waliwaelekeza watalaam wa Wizara ya Nishati kutoka Tanzania na DRC pamoja na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa pamoja waandae  mpango kazi wa kutekeleza makubaliano hayo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Watalaam wa Wizara ya Nishati ya Tanzania na DRC, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa  Tanzania nchini DRC na TPDC.

Waziri wa Nishati wa DRC, pia alipata fursa ya kutembelea miundombinu ya kupakulia mafuta katika Gati ya Kurasini, SPM na baadaye kutembelea miundombinu ya bomba la Tazama ili kupata ufahamu kuhusu uendeshaji wa Bomba hilo refu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama