Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Dkt. Kalemani Aagiza Mitaa Yote ya Majiji Kuwa na Umeme Ifikapo Juni 30

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akionyesha nyumba ambazo  bado hazijaunganishiwa umeme katika eneo la Ntyuka jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kukagua maeneo ya mijini ambayo hayana umeme. Wengine katika picha ni watendaji wa TANESCO na Wizara ya Nishati.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewaagiza Watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2019, mitaa yote isiyo na umeme katika Majiji yote nchini iwe imesambaziwa umeme.

Dkt Kalemani aliyasema hayo tarehe 5 Mei, 2019, mara baada ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma ambayo bado yana nyumba nyingi ambazo hazijaunganishwa na umeme.

Katika ziara hiyo aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka, Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

” Mwisho wa kuunganisha umeme kwenye maeneo haya ya Majiji ni Juni 30 mwaka huu, iwe Ntyuka, Mkonze, jijini Dodoma, au Murieti jijini Arusha, haya maeneo yana kero ya umeme lazima yapatiwe nishati hii haraka ili yafanane na hadhi ya Majiji hivyo jukumu la mwananchi ni kufanyawiring na kulipia huduma ya umeme.” alisema Dkt Kalemani.

Dkt. Kalemani alisema kuwa kazi ya uuganishaji umeme katika mitaa isiyo na umeme katika mikoa mingine ambayo si majiji itaendelea hadi mwezi Desemba mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufanya ziara ya kukagua maeneo ya mijini ambayo hayana umeme. Wengine katika picha ni watendaji wa TANESCO na Wizara ya Nishati.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikagua maeneo ambayo hayajaunganishwa na umeme katika eneo la Mkonze jijini Dodoma.Wengine katika picha ni watendaji wa TANESCO na Wizara ya Nishati.

Aidha, Waziri wa Nishati aliwataka Wataalam kutoka TANESCO kutokataa malipo ya wananchi wanaotaka kuunganishiwa umeme bali wanapaswa kupokea malipo hayo na kuwasambazia umeme wateja.

Kabla ya kufanya ziara hiyo, Waziri wa Nishati, alifanya kikao na watendaji wa TANESCO ambapo pamoja na kuwapongeza kwa jitihada mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha na uhakika, aliwata kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za umeme zinazoendelea kujitokeza.

Dkt. Kalemani alisema kuwa moja ya changamoto wanayopaswa kushughulikia ni kuunganishia umeme wateja waliolipia huduma ya umeme na hawajaunganishwa kwa muda mrefu ambapo aliagiza kuwa mwisho wa kuwaunganishia umeme wateja hao ni mwezi wa Tano mwaka huu.

Aidha aliiagiza TANESCO kuhakikisha kuwa, ifikapo mwisho wa mwezi wa Tano mwaka huu, maeneo yaliyounganishwa na umeme wa gridi yanapata umeme wa kutosha na wa uhakika ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali bila kikwazo cha uwepo wa nishati ya kutosha.

20 thoughts on “Dkt. Kalemani Aagiza Mitaa Yote ya Majiji Kuwa na Umeme Ifikapo Juni 30

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama