Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Dkt.Abbasi Atunukiwa Cheti cha Uprofesa, Akumbusha Wajibu wa Wanahabari Katika Maendeleo ya Nchi

Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akielezea mada kwa wanafunzi wa Kitivo cha Lugha na Utamaduni wa Kigeni wa Chuo Kikuu cha Mawasiliano na Habari cha China (China Communication University), (Hawapo pichani).

Na Beatrice Lyimo- CHINA

Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi ametunukiwa cheti cha Uprofesa wa Muda (Part Time and Research Professor) katika Kitivo cha Lugha na Utamaduni wa Kigeni katika Chuo Kikuu cha Mawasiliano na Habari cha China (China Communication University).

Tuzo hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitivo hicho kwa kutambua mchango wa Dkt. Abbasi katika tasnia ya habari, utafiti na lugha ya Kiswahili.

Akizungumza wakati wa hotuba yake chuoni hapo kuhusu hali ya sekta ya habari nchini Tanzania, Dkt. Abbasi amesema kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kusaidia maendeleo ya nchi na kuwa chachu ya amani na si vurugu.

“Sisi kama wanahabari au vyombo vya habari tunapaswa kuwa na  weledi na wajibu wetu mkuu ni kusaidia maendeleo ya nchi na si kuzigawa jamii au kuzitofautisha. Waandishi wa habari wa hapa China ni mfano mzuri wa kile ninachokiita uandishi wa habari za kimaendeleo na si za kimapokeo ” amefafanua Dkt. Abbasi.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akifafanua mada mbalimbali za Tanzania wanafunzi wa Kitivo cha Lugha na Utamaduni wa Kigeni katika Chuo Kikuu cha Mawasiliano na Habari cha China (China Communication University).

Aidha, Dkt. Abbasi ameshauri vyombo vya habari nchini Tanzania kutobaki na mfumo mmoja wa utoaji taarifa bali kujiimarisha katika mifumo mingine ya kidigitali kwani dunia imehama kutoka analojia kwenda digitali.

Hata hivyo, kabla ya kuhutubia wanafunzi wa kitivo cha utamaduni na lugha za kigeni chuoni hapo, Dkt. Abbasi alipata fusra ya kuzungumza na Naibu Mkuu wa Chuo Prof. Zhang Shu Ting na kuahidiana kushirikiana katika mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya habari na mawasiliano.

“Urafiki kati ya China na Tanzania utadumu daima, kutokana na faida tunazozipata kati yetu sisi tutafanya kila jitihada kushirikiana nanyi” ameongeza Dkt. Ting.

Wanafunzi wa Kitivo cha Lugha na Utamaduni wa Kigeni katika Chuo Kikuu cha Mawasiliano na Habari cha China (China Communication University) wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (hayupo pichani) wakati wa majadiliano juu ya mada mbalimbali zinazohusu nchi ya Tanzania.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Kitivo cha Lugha na Utamaduni wa Kigeni katika Chuo Kikuu cha Mawasiliano na Habari cha China (China Communication University) wakiwa wamebeba majarida waliyokabidhiwa na Dkt. Abbasi yakiwa yameandikwa kwa lugha ya kiswahili.

Jumla ya Watanzania 22 wameshamaliza masomo yao katika chuo hicho pekee kinachotoa masomo yake kwa lugha ya Kiingereza nchini China ambapo hadi sasa Watanzania wanaoendelea na masomo ni 7.

Chuo cha Mawasiliano cha China kilianzishwa mwaka 1964 na ni moja ya vyuo vya kimataifa  vinavyotoa masomo ya habari na mawasiliano.

Katika ziara hiyo, Dkt. Abbasi ameambatana na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano kutoka taasisi mbalimbali za umma nchini Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama