Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

China na Tanzania Kushirikiana Katika Mafunzo kwa Wanahabari

Msemaji Mkuu wa Serikali na ujumbe wake akiwa katika mazungumzo na maafisa katika wizara ya Mambo ya Nje ya China jijini Beijing jana.

Na: Beatrice Lyimo – CHINA

Kansela wa Idara ya Habari, Wizara ya Mambo ya Nje katika Jamhuri ya Watu wa  China, Bw. Gong Anmin amemuahidi Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi kushughulikia suala la mafunzo kwa Wanahabari wa Tanzania kwa lengo la kuwajengea uwezo katika sekta ya mawasiliano.

Bw.Gong ameyasema hayo wakati wa mkutano maalumu baina yake na ujumbe kutoka Tanzania ulioongozwa na Dkt. Abbasi uliolenga kujifunza na kubadilishana uzoefu katika sekta ya habari na mawasiliano na wataalamu wa Serikali ya China.

Bw. Gong aliongeza kuwa: “suala la kuongeza uwezo kwa wanahabari ni muhimu kwani itasaidia kuongeza taaluma waliyonayo hivyo nitajitahidi kufanikisha mafunzo kwa wanahabari wa Tanzania ambayo ni nchi rafiki na China kwa miaka mingi”

Mbali na hayo Dkt. Abbasi pia amekutana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje anayeshughulikia Idara ya Masuala ya Afrika Bw. WAN Li.

Katika Mazungumzo yao Bw. Wan amesema kuwa urafiki wa Tanzania na China ni wa muda mrefu na ulianzishwa na waasisi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong hivyo kuahidi kutunza na kudumisha urafiki huo.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt.  Hassan Abbasi akimkabidhi jarida la NCHI YETU Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ambaye alikuwa akisaidia kufanya ukalimani kutoka lugha ya Kichina hadi Kiswahili kama ishara ya kumsaidia kuongeza ujuzi wake zaidi katika lugha ya Kiswahili.

Bw. Wan anaongeza kuwa katika miaka 54 iliyopita uhusiano wa kibalozi baina ya nchi hizo umezidi kuimarishwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.

Aidha, Bw. Wan alieleza kufurahishwa na mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea nchini Tanzania na kusema wanayaunga mkono.

Kwa upande wake, Dkt. Abbasi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuzidi kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Dkt. Abbasi aliongeza kuwa baada ya mikataba mingi ya ushirikiano kuasisiwa miaka ya nyuma Serikali ya sasa ya Tanzania pia ilisaini mkataba mpya wa ushirikiano katika sekta za utamaduni na habari na Serikali ya China  mwaka 2016 unaoshadidisha zaidi urafiki kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha Dkt. Abbasi amesema kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea Tanzania ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa nchini Tanzania (SGR) hivyo amewakaribisha wawekezaji kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuwekeza katika miundombinu ya sekta ya reli lakini pia kuwaalika Wachina kutembelea Tanzania na kufaidika na maeneo mbalimbali ya utalii.

76 thoughts on “China na Tanzania Kushirikiana Katika Mafunzo kwa Wanahabari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama