Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

GCLA Watakiwa Kuandaa Mkataba wa Utoaji Huduma

Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile (kulia) akiongea wakati wa uzinduzi wa Bodi Tendaji ya kwanza ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Mkemia, Dar es Salaam. Kushoto (waliokaa) ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Esther Hellen Jason na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko.

Na Jacquiline Mrisho.

Bodi Tendaji ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetakiwa kuandaa mkataba wa utoaji huduma ili kuepuka ucheleweshaji katika utoaji wa majibu kwa wananchi wanaohitaji huduma za mamlaka hiyo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo yenye jumla ya wajumbe saba.

“Mamlaka hii ni nyeti sana kwa hiyo tunatakiwa kuwa na mkataba wa utoaji wa huduma ili mtu akileta sampuli zake hapa afahamu lini atapata majibu hivyo kujiondoa kuwa sehemu ya ucheleweshaji wa utoaji wa haki,” alisema Dkt. Ndugulile.

Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi Tendaji ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Esther Hellen Jason (wa pili kulia) Sheria na kanuni zake zinazosimamiwa na Mamlaka ikiwa ni ishara ya kuizindua rasmi Bodi hiyo. Wengine katika picha ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Otilia Gowele (mwenye koti jeupe) na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (wa kwanza kulia).

Aidha,Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa ni lazima kuwa na ithibati kutokana na umuhimu wa Mamlaka hiyo kwani imepewa jukumu la kisheria kusimama Mahakamani kutoa majibu sahihi juu ya uchunguzi fulani hivyo ni lazima apatikane mtu wa kusimamia ubora ili majibu yanayotolewa yawe yanaaminika na kuweza kutumika ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa Mamlaka imepata sheria mpya, muundo mpya, uongozi mpya pamoja na bodi mpya, hivyo imepewa meno ya kisheria katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu pamoja na kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko ameiomba Serikali kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo zikiwemo za upungufu wa watumishi 172 pamoja na kununua mitambo ya kisasa kwani mitambo iliyopo haiendani na hali halisi.

Mameneja na wakuu wa Vitengo wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa Bodi Tendaji ya Kwanza ya Mamlaka hiyo ambayo imezinduliwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile leo kwenye ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) akiwa pamoja na Wajumbe wa Bodi Tendaji ya Kwanza ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Kaimu Katibu Mkuu (Afya), Dkt. Otilia Gowele (wa pili kutoka kushoto) na Mwanasheria kutoka Wizara ya Afya, Bi. Tunu Temu( wa kwanza kushoto).

Vile vile amemuahidi Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa ataendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ikiwemo suala la kuhamia jijini Dodoma.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Esther Hellen Jason amemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua katika nafasi hiyo ambapo amesema bodi itafanya kazi kwa weledi na kujituma ili kufikia matarajio ya nchi kama yalivyopangwa.

 

 

112 thoughts on “GCLA Watakiwa Kuandaa Mkataba wa Utoaji Huduma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama