Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Ndege Mpya Aina ya Bombardier Dash 8 Q400 Yapokelewa Nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 30 Julai, 2021 ameongoza Watanzania katika mapokezi ya Ndege mpya aina ya Bombardier Dash 8 Q400 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.


Kuwasili kwa Ndege hiyo iliyotokea nchini Canada kunaongeza idadi ya Ndege zilizonunuliwa na kuwasili kufikia 9 kati ya 11, Ndege nyingine 2 zinatarajiwa kuwasili mwezi Oktoba 2021.


Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea Ndege hiyo, Mhe. Rais Samia amesema usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha maendeleo Duniani kwa sababu usafiri huo ni wa haraka, salama na wenye kutumiwa na watu wengi.


Mhe. Rais Samia amesema mbali na usafiri wa anga kusafirisha Watu, pia ni muhimu katika kusafirisha bidhaa mbalimbali, hususan zinazoharibika haraka kama vile matunda, mbogamboga, samaki, maua, nyama na nyinginezo.


Amesema Serikali imeamua kununua Ndege ya kusafirisha mizigo kwasababu nchi yetu ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa matunda, mbogamboga na maua, ambapo mwaka 2019, Tanzania iliuza Nje mazao yenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani milioni 700 na ina tarajia hadi kufikia mwaka 2025 kuingiza Dola za Marekani bilioni 2.


Aidha, Mhe. Rais Samia amesema ili nchi iweze kuvutia watalii wengi na kunufaika nao ni lazima iimarishe usafiri wa anga na ndio sababu Serikali iliamua kufufua Shirika la Ndege la ATCL ikiwa na malengo ya kupokea watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2019.


Amesema Serikali imeamua kuimarisha huduma za usafiri nchini ili iweze kunufaika na fursa za kijiografia za kupakana na nchi 8, ambapo kati ya hizo 6 hazina Bahari.


Mhe. Rais Samia amezihimiza Wizara za Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji na Sekta Binafsi kuweka mikakati ya kunufaika na fursa hizo ikiwemo kuanzisha kongani za kiuchumi kwenye maeneo ambapo miundombinu ya usafiri inajengwa.


Vilevile Mhe. Rais Samia ameipongeza ATCL kwa kuimarika tangu ilipofufuliwa ambapo idadi ya watu wanaosafiri kwa Ndege za shirika hilo imeongezeka kutoka wastani wa abiria 4000 hadi 60,000 kwa mwezi.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imeongeza safari za kimataifa kutoka kituo kimoja cha Comoro hadi saba ambavyo ni Burundi, China, India, Uganda, Zambia, Zimbabwe na hivi karibuni inatarajiwa kuanzisha safari katika miji ya Kinshasa, Lubumbashi, Kalemie, Ndola, Nairobi, Dubai, Muscat, na London.


Mapokezi ya ndege hiyo mpya pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamella O’Donell, viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na viongozi mbalimbali wa dini na vyama vya siasa.

Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Rais Samia Apokea Ujumbe Maalum Kutoka kwa Rais Tshisekedi wa Congo

Usikivu wa TBC Wapanda kwa Asilimia 14 Ndani ya Miezi Miwili

Na John Mapepele, WHUSM

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,. Mhe Innocent Bashungwa amesema hadi kufikia Mwezi Septemba, mwaka  huu usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utapanda kuzifikia Wilaya 120 sawa na 76%  kutoka Wilaya 103  ambapo ni sawa na 64% za usikivu wa sasa ili kuhahakikisha wananchi wote wanapata habari kwa uhakika.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Julai 30, 2021 kwenye uzinduzi wa kituo cha kurushia matangazo ya redio eneo la Kisaki mkoani Morogoroambapo amesema katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, TBC inatekeleza miradi ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya za Karagwe (Kagera), Same (Kilimanjaro), Sikonge (Tabora), Kahama (Shinyanga), Bunda (Mara), Nkasi (Rukwa) na Kasulu (Kigoma)ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa miradi hii kutawezesha usikivu wa TBC kufikia 76% ya nchi nzima.

“Nataka kuwahakikishia wananchi wote kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi shupavu wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kupanua usikivu wa redio za TBC nchi nzima” amesisitiza Mhe. Bashungwa

Wananchi Muleba Waiomba Serikali Kuwafikishia Mawasiliano ya Redio na Simu

Na Faraja Mpina, MULEBA

Wananchi wa Wilaya ya Muleba wameiomba Serikali kuwafikishia huduma za mawasiliano ya redio na simu wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wilayani humo

Kwa nyakati tofauti wananchi wamezungumzia hisia zao za kukosa mawasiliano ya redio za Tanzania hasa redio ya Taifa TBC na matokeo yake wanasikiliza redio za nchi jirani ya Rwanda hivyo kushindwa kuelewa nini kinaendelea ndani ya nchi yao

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya hiyo imeshaanza mchakato wa kuanzisha redio ya jamii lakini mchakato umekuwa mrefu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivyo kumuomba Naibu Waziri huyo kuingilia kati suala hilo ili redio hiyo ianzishwe na kuanza kuwahudumia wananchi wa Muleba

Mradi wa Umeme wa Ujazilizi Mkoani Kilimanjaro Wazinduliwa Same

 Na Zuena Msuya, Kilimanjaro

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua mradi wa umeme wa Ujazilizi Fungu la Pili kwa Mkoa wa Kilimanjaro na kuagiza kukatwa 10% ya malipo ya wakandarasi Kampuni ya NJARITA na OCTOPUS kwa kutokamilisha Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) mkoani humo.

Aidha, ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Same kumsaka na kumuweka ndani mkandarasi NJARITA kwa kutokuwepo eneo la mradi.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo wakati akizindua mradi huo uliofanyika wilayani Same kwa kuwasha umeme katika Kijiji cha Muheza Kata ya Maore, Nasuro Kata ya Mwembe wilayani humo, Julai 29, 2021.

Naibu Waziri Dkt. Mabula Amaliza Utata Mpaka wa Masasi na Newala

Na Munir Shemweta, MTWARA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amemaliza utata wa muda mrefu kuhusiana na mgogoro wa mpaka kati ya wilaya ya Masasi na Newala mkoani Mtwara baada ya kubainisha mpaka halisi baina ya pande hizo mbili.

Akiwa ameambatana na wataalamu wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mtwara, Wakuu wa Wilaya za Masasi na Newala, Wabunge pamoja na Wakurugenzi wa Hlmashauri zinazopakana ikiwa ni utelelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, Dkt. Mabula alibainisha mpaka halisi uliopo kati ya kijiji cha Njenga na Miyuyu ikiwa ni takriban kilometa tano kutoka ulipoainishwa mpaka wa awali.

Akizungumza wakati wa usuluhishi wa mgogoro huo Julai 28, 2021 Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Mabula alisema, jambo kubwa lililotatiza kwenye  mgogoro huo wa mpaka ni uhitaji wa maeneo ya kiutawala ambapo upande wa wakuu wa wilaya alisema hawakuwa na tatizo.

Serikali Kutumia Bilioni 1 na Milioni 15 Kupeleka Mawasiliano Mbogwe

Na Faraja Mpina, MBOGWE

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 1,015,000,000 kufikisha huduma ya mawasiliano katika Wilaya ya Mbogwe iliyopo Mkoani Geita kupitia zabuni zilizotangazwa na Mfuko huo Juni 30 mwaka huu.

Hayo ameyazungumza Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya hiyo ambapo alizungumza na uongozi wa Wilaya hiyo pamoja na wananchi na kuwahakikishia kuwa Serikali itawafikishia huduma ya mawasiliano kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha 2021/22

Mhandisi Kundo amesema kuwa ndani ya Wilaya ya Mbogwe, Minara mitano ya mawasiliano itajengwa na watoa huduma kupitia zabuni zilizotangazwa na UCSAF ili wananchi wa Wilaya hiyo waweze kupata huduma za mawasiliano kwa sababu mawasiliano yanasaidia kukuza uchumi, kuimarisha ulinzi na usalama na husaidia katika mazingira ya dharura

ev eşyası depolama