Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Biteko Abaini Masanduku 209 ya Sampuli za Madini Yaliyotelekezwa

Sehemu ya masanduku 209 yenye sampuli za madini mbalimbali yaliyotelekezwa na kampuni ya Sino Hydro kutoka China, nyumbani kwa Allan Mbilinyi katika kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Na Greyson Mwase, Songea

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo amefanya ziara katika Mkoa wa Ruvuma lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo pamoja na kusikiliza kero mbalimbali.

Katika ziara yake aliambatana na  wataalam kutoka Wizara ya Madini, Maafisa Madini wa Songea, Kulwa Kabadi na Mhandisi George Wandinha, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Songea.

Akiwa katika eneo la Madiba lililopo wilayani Songea mkoani Ruvuma, Naibu Waziri Biteko alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa mwananchi mmoja, Allan Mbilinyi kunakoelezwa kuhifadhiwa masanduku 209 ya sampuli za madini ya aina mbalimbali na kushuhudia masanduku hayo yakiwa yametelekezwa bila kuwa na dalili za aina yoyote ya usafirishwaji.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akimsikiliza Allan Mbilinyi (wa pili kushoto) ambaye masanduku 209 yenye sampuli za madini mbalimbali yalitelekezwa na kampuni ya Sino Hydro kutoka China, nyumbani na kwake katika kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Awali Naibu Waziri Biteko alipewa taarifa na wananchi ambao ni wasamaria wema kutoka katika eneo la Madaba juu ya uwepo wa sampuli za madini hayo na kusisitiza kuwa  hatua hiyo inatokana na kuunga mkono kasi ya Serikali ya Awamu ya  Tano kupitia  Wizara ya Madini kwenye ulindaji  wa  rasilimali za madini.

Walisema kuwa, tofauti na sampuli za masanduku 209 ya madini ya aina mbalimbali yaliyotelekezwa, kipindi cha nyuma walishuhudia mzigo mkubwa wa masanduku yenye sampuli za madini ya aina mbalimbali yakisafirishwa kutokea eneo yalipotelekezwa masanduku husika.

Naye Naibu Waziri Biteko aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa za madini yaliyotelekezwa alielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia na kumpatia taarifa kabla ya kufika na kuthibitisha na kusisitiza kuwa aliamua kufika ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua za kisheria.

Hata hiyo baada ya kufika eneo husika, Waziri Biteko aliangalia mkataba uliosainiwa kati ya kampuni ya Sino Hydro kutoka China na Allan Mbilinyi kuhusu uhifadhi wa madini hayo na kubaini kutokuwepo kwa kibali cha serikali jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akizungumza na wananchi wa Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (kulia) kabla ya kuanza ziara yake katika mkoa huo.

“Ni kosa la kisheria kuhifadhi madini ya aina yoyote ndani ya mahali popote bila ya Serikali kuwa na taarifa, faini yake ni kubwa pamoja na kifungo,” alisema Biteko

Biteko alielekeza sampuli za madini kuwa chini ya uangalizi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema kabla ya kukabidhiwa kwa Wakala wa Utafiti wa Madini na Jiolojia Tanzania (GST) kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini thamani halisi.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini katika ufuatiliaji wa madini na kusisitiza kuwa Serikali itahakikisha wahusika wanakamatwa sehemu yoyote na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma, Biteko mbali na kuwapongeza wananchi kwa uzalendo wa kutoa taarifa kuhusiana na uhalifu unaofanywa na watu wasio waaminifu kwenye sekta ya madini, aliwataka wananchi hao kuendelea kulinda rasilimali za madini na kusisitiza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha Naibu Waziri Biteko akizungumza kwa nyakati tofauti katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme alisema kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la  Taifa ikiwa ni pamoja na maboresho ya Sheria ya Madini inayomtambua mtanzania kama mmiliki wa madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini nje ya nchi.

Aliwataka wachimbaji madini wanapopata leseni kujitambulisha kwanza kwa viongozi kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na kijiji pamoja na kulipa fidia kwa wananchi  kabla ya kuanza shughuli zozote za madini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisema kuwa atafuatilia kila hatua ya namna taarifa zilivyofikishwa Serikalini kuhusu madini yaliyotelekezwa na hatua zilizochukuliwa pamoja na wahusika wote kabla ya  hatua za kisheria kuchukuliwa.

Wakati huohuo Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama alimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa ya usimamizi  wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa karibu shughuli za madini kwa kila mkoa na kuchukua  hatua stahiki pale inapohitajika.

 

 

 

 

 

48 thoughts on “Biteko Abaini Masanduku 209 ya Sampuli za Madini Yaliyotelekezwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama