Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

BAKITA Yaanzisha Mfumo wa Kutunza Taarifa za Wataalam wa Kiswahili Nchini.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) Dkt. Seleman Sewangi (katikati) akifafanua jambo kuhusu kuanzisha utaratibu wa kuhifadhi taarifa za wataalam wa kiswahili(Kanzi data) alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utamaduni Wizara ya Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi.Shani Kitogo kutoka kushoto ni Kaimu Ofisa Mawasiliano wa Baraza hilo Bi. Consolata Mushi.

Na.Paschal Dotto.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limeanzisha mchakato wa ukusanyaji taarifa za wataalam wa Kiswahili na kiziweka katika mkusanyiko maalumu wa habari (Kanzidata) ili watakapohitajika wapatikane kwa urahisi.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt. Seleman Sewangi  amesema siku zijazo uhitaji wa Kiswahili utakuwa mkubwa duniani kwa hiyo wataalam wa Kiswahili ni fursa kwao ili kuwapatia ajira lakini pia kukuza lugha ya Kiswahili.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi.Shani Kitogo akisisitiza jambo kuhusu kuanzisha utaratibu wa kuhifadhi taarifa za wataalam wa kiswahili (Kanzi data) alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) Dkt. Seleman Sewangi.Picha na Paschal Dotto.

“Ni aibu kwa nchi kubwa kama yetu yenye utajiri mkubwa na weledi katika Kiswahili isiweze kuuza watu wake, na pia haiwezi kuwauza kama haijui waliko, haijui wanafanya nini pamoja na kujua viwango vyao vya taaluma ili kuweza kuwatafutia fursa za kufundisha Kiswahili katika mataifa yenye uhitaji, hivyo BAKITA ikaona nivyema kutengeneza kanzidata hiyo”, alisema Dkt.Sewangi.

Alisema kuwa lugha ya Kiswahili kwa sasa ina mahitaji makubwa duniani kwa hiyo wataalam waliobobea katika lugha wenye kunanzia ngazi ya shahada ya Kiswahili na kuendelea watume taarifa zao kwenda kwenye barua pepe ya Baraza la Kiswahili la Taifa ambayo ni bakita@habari.go.tz na maombi yao yatapokelewa na kufanyiwa kazi.

Hivi karibuni katika ziara za wakuu wa nchi mbalimbali walizofanya hapa nchini, mfano ziara ya Rais wa Misri Abdel Fattah Elsisi ambaye aliomba waalimu wa lugha ya Kiswahili kwenda kufundisha Kiswahili nchini Misri, maombi hayo yameleta chachu na hamasa kwa wataalam wa Kiswahili kwamba wanahitajika sio tu kitaifa bali hata kimataifa na huo ndio mwanzo wa kupanuka kwa fursa za ajira kwa wataalam hao.

Katibu Mtendaji huyo wa BAKITA alivitaja vitu vinavyohitajika ili mtaalam wa Kiswahili aweze kuingizwa kwenye kanzidata kuwa ni vivuli vya vyeti vya matokeo ya kuhitimu vyuo vikuu na katika taasisi nyingine za mafunzo husianifu kama vile utalaamu wa ukalimani,tafsiri, ualimu wa Kiswahili kwa wageni.

Vigezo vingine ni utaalam katika ukalimani wa lugha ya alama kwa Kiswahili pamoja na wasifu wa wataalamu hao wenye taarifa zingine kama vile namba za simu,anuani za barua pepe, hali yao ya ajira, lugha zingine za kimataifa wanazozijua na uzoefu wao katika ajira zinazohusiana na Kiswahili.

Aidha Dkt. Sewangi amewataka wataaluma hao kuwa wasitume taarifa ambazo hazihitajiki katika mchakato huo bali watume kama tangazo linavyoelekeza.

Dkt.Sewangi amesema BAKITA haihusiki na ajira bali kutunza taarifa za wataaluma na wataalam wa Kiswahili kwa mahitaji na fursa za siku zijazo katika nchi mbalimabali duniani zinazohitaji wataalam wa Kiswahili.

“BAKITA haihusiani na ajira bali ina dhamana ya kutunza kanzidata ili serikali ijue ina wataalam wangapi na mahali walipo kwaajili ya kuwaunganisha na wahitaji hivyo hatuhusiki na mchakato wowote wa kuwatafutia watu ajira”, alisisitiza Dkt.Sewangi.

Wataalam wa Kiswahili watakaopata ajira sehemu mbalimbali duniani watasaidia sio tu kuitangaza na kuikuza lugha hiyo bali watasaidia katika kuongeza pato la taifa kwani katika asilimia ya malipo watakayopata Serikali na yenyewe itanufaika na kiasi Fulani.

Mchakato wa kuwapata na kuwaweka wataalam wa Kiswahili kwenye kanzidata utaendelea hadi mwezi Septemba mwaka huu na hadi sasa BAKITA imepokea maombi ya wataalam takribani 60.

 

54 thoughts on “BAKITA Yaanzisha Mfumo wa Kutunza Taarifa za Wataalam wa Kiswahili Nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama