Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Afreximbank Kuipatia Tanzania Zaidi ya Trilioni Moja Kugharamia Reli na Vituo vya Biashara

Na: WFM,  Mjini Bali Indonesia

African Export Import Bank (Afreximbank) ya Misri, imeonyesha nia ya kuipatia Tanzania mkopo wa zaidi ya Shilingi trilioni moja (dola za Marekani zaidi ya milioni 500) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kipaumbele hasa ya miundombinu ya reli na kujenga vituo vya biashara (SEZ and Industrial parks).

Hayo yalibainishwa mjini Bali Indonesia, na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango baada ya Mkutano na Makamu wa Rais wa Afreximbank Bw. Amr Kamel,  uliofanyika  wakati wa mikutano ya mwaka  ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ikiendelea.

Waziri Mpango, alisema kuwa Afreximbank imethibitisha kuwa ipo tayari kutoa mkopo wa  dola za Marekani milioni 125  (takribani Shilingi bilioni 285.9) kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa  (SGR),  kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma.

“Afreximbank wanania pia ya kutoa  dola milioni 400 (takribani Sh. Bilioni 914.9) ambazo wanaweza kutukopesha kwa ajili ya kugharamia miradi ya miundombinu itakayorahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani na Bara la Afrika kwa ujumla,  ili kuchochea kasi ya ukuaji wa biashara katika nchi hizo kwa lengo la kuondoa umasikini”, aliongeza Dkt. Mpango.

Alisema kuwa kwa kuwa tayari Tanzania ilikuwa na mkakati wa kufungua vituo vya biashara katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na mikoa mingine, suala la mkopo huo ni fursa kubwa kwa  maendeleo ya nchi, hivyo jambo hilo litafanyiwa kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji  na Sekta Binafsi, ili Taifa liweze kunufaika na fedha ambazo benki hiyo ipo tayari kuzitoa.

Aidha, amesema kuwa  katika majadiliano na benki hiyo kuna umuhimu wa kuangalia namna ya rasilimali fedha ambazo Benki Kuu za nchi mbalimbali za Afrika zimekuwa zikiwekeza nje ya Bara hilo, ili ziweze kuwekezwa kwenye benki za Afrika kama Afreximbank ili kuleta maendeleo kwa haraka katika Bara hilo.

Vile vile benki hiyo imeikaribisha Tanzania kushiriki mkutano wa biashara utakaofanyika mwezi Desemba mwaka huu mjini Cairo Misri, ambapo kwa upande wa Tanzania ni fursa kwa Makampuni ya umma na binafsi kutangaza bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kwa lengo la kukuza biashara ndani ya Bara la Afrika.

Makamu wa Rais wa Afreximbank Bw. Amr Kamel, alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za kimkakati kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi jirani, hivyo Afreximbank imeamua kusaidia miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ili kuharakisha maendeleo ya nchi ya Tanzania na nyingine.

Waziri Dkt. Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa kuisaidia Tanzania katika mkakati wa kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025, hivyo kuwa Taasisi yenye tija si tu kwa maendeleo ya Tanzania lakini pia kwa Bara la Afrika.

Imetolewa na :-

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha na Mipango

                                              Bali, Indonesia

68 thoughts on “Afreximbank Kuipatia Tanzania Zaidi ya Trilioni Moja Kugharamia Reli na Vituo vya Biashara

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama