Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wilaya Zenye Majimbo Mawili Ziangaliwe kwa Umakini Katika Upangaji wa Miradi ya Umeme Vijijini – Mgalu

Na Teresia Mhagama, Ruvuma

 Naibu Waziri wa Nishati, Subira  Mgalu, amewataka wataalam katika Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa makini katika kazi ya upangaji wa vijiji vinavyopaswa kupelekewa umeme kwenye wilaya zenye majimbo mawili ya uchaguzi ili kuepusha malalamiko ya kupendelea upande mmoja wa Wilaya.

Aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akikagua miradi ya usambazaji umeme vijijini katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambapo Wilaya hiyo ina Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada ya kupata malalamiko kuwa, Vijiji vingi vya Tunduru Kaskazini ndivyo vimesambaziwa umeme huku Tunduru Kusini ikiwa na Vijiji vichache

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika Kijiji cha Mtakanini, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.

Aidha, Naibu Waziri aliagiza kuwa, kazi ya upangaji wa Vijiji vinavyotarajiwa kupelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali ishirikishe viongozi wa ngazi mbalimbali katika maeneo ili kuondoa malalamiko katika miradi hiyo.

Vilevile alisema kuwa, wataalam hao wahakikishe kuwa hawaruki Vijiji na badala yake kila kijiji kinachopitiwa na mradi kisambaziwe nishati ya umeme.

Kuhusu kazi ya uunganishaji Wilaya ya Tunduru  kwenye umeme wa gridi,  Naibu Waziri alisema kuwa, wilaya hiyo itaanza kupata  umeme huo kuanzia mwezi Machi mwakani baada ya kuvuta umeme kutokea wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akiwa wilayani Tunduru, Naibu Waziri, aliwasha umeme katika Kijiji cha Namiungo, Mchuluka, Kangomba na Daraja Mbili ambapo kaya zaidi ya 100 zimeunganishwa na huduma hiyo ikiwemo vituo vya afya na shule.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi, (hawapo pichani) kabla ya kuzindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Namtumbo, Eng. Edwin Ngonyani na kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Mfaume.

Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Hanga, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati alipofika kijijini hapo kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini na kuwasha umeme katika Kijiji hicho.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi baada ya kuwasha rasmi umeme katika Kijiji cha Mchuluka wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri pia alifanya ziara katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini, aliwasha umeme katika Kijiji cha Migelegele, Mtakanini na Hanga.

Baada ya umeme kufika  katika vijiji hivyo, jumla ya kaya 105 zimesambaziwa umeme huo zikiwemo Taasisi za umma na sehemu za ibada huku kazi hiyo ya uunganishaji umeme inaendelea.

Wananchi mbalimbali katika vijiji vilivyosambaziwa umeme waliishukuru Serikali kwa kuwasambazia umeme huo ambao umewawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kupata huduma za matibabu hata nyakati za usiku tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

64 thoughts on “Wilaya Zenye Majimbo Mawili Ziangaliwe kwa Umakini Katika Upangaji wa Miradi ya Umeme Vijijini – Mgalu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama