Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mfumuko wa Bei Mwezi Agosti Wabaki Asilimia 3.3

1. Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraim Kwesigabo akitangaza hali ya Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2018 leo jijini Dodoma.

Na: Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA

Ofisi ya Taifa ya Takwimu ‘NBS’ imetoa taarifa ya mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2018 ambapo imeelezwa kuwa Mfumuko huo umebaki kuwa asilimia 3.3 kama iliyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018.

Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo  amesema kuwa, hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioisha wa mwezi Agosti,2018 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018.

Baadhi ya waandishi wa Habari walioshiriki kwenye ‘Press Conference’ ya kutangazwa kwa hali ya Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2018 leo jijini Dodoma. (Picha na: MAELEZO)

Aidha, Kwesigabo ameeleza sababu za mfumuko wa bei wa mwezi agosti, 2018 kubaki kuwa sawa kama mwezi Julai, 2018 kuwa umechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Agosti, 2018 zikilinganishwa na Bei za mwezi Agosti, 2017 pamoja na kuongezeka kidogo kwa bidhaa zisizo za chakula.

“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia mfumuko wa bei wa mwezi Agosti, 2018 kubaki sawa kama ilivyokuwa mwezi Julai, 2018 ni pamoja na kupungua kwa unga wa mahindi kwa asilimia 11.2, mtama kwa asilimia 18.1, unga wa mihogo kwa asilimia 13.9, maharagwe kwa asilimia 3.4 na magimbi kwa asilimia 17.4”

“Hata hivyo kuna baadhi ya bidhaa zilionesha mwenendo wa kupanda kama dizeli kwa asilimia 23.0, petroli kwa asilimia 16.7, mafuta ya taa kwa asilimia 19, nguo kwa asilimia 2.9 na viatu kwa asilimia 2.2” amefafanua Kwisegabo.

Kwa upande wa hali ya mfumuko kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, Kwesigabo ameeleza kuwa, nchini Uganda mfumuko kwa mwaka wluioishia mwezi Agosti, 2018 umeongezeka hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 3.1 kwa mwezi Julai, 2018 na kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwezi Agosti, 2018 umepingua hadi asilimia 4.04 kutoka asilimia 4.35 kwa mwezi Julai, 2018.

NBS imepewa mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji wa Takwimu rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za mfumuko wa bei kwa ajili ya matumizi ya serikali na wadau wa takwimu ambapo mfumuko wa bei wa taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bishaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

 

 

40 thoughts on “Mfumuko wa Bei Mwezi Agosti Wabaki Asilimia 3.3

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama