Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mfumuko wa Bei Washuka na Kufikia Asilimia 3.8

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari(hawapo pichani) alipokuwa akiongelea mfumuko wa bei leo Jijini Dar es Salaam. Mfumuko wa bei wa Taifa umeshuka toka asilimia 3.9 mwezi Machi hadi kufikia 3.8 Aprili.

Na. Eliphace Marwa

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Aprili, 2018 umepungua hadi kufikia asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.9 ilivyokuwa mwezi Machi, 2018.

Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2018 imepungua  ikilinganishwa na mwezi Machi, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa  Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Aprili, 2018 kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu mfumko wa bei wa Taifa leo Jijini Dar es Salaam, Mfumuko wa bei umeshuka toka asilimia 3.9 mwezi Machi hadi kufikia 3.8 Aprili. Kulia ni Meneja wa Ajira na Bei toka NBS, Ruth Minja.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Aprili kumechangiwa na kushuka kwa gharama za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Aprili, 2018 zikilinganishwa na bei za mwezi Aprili, 2017”, alisema Bw. Kwesigabo.

Alitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na mahindi kupungua kwa asilimia 5.2, unga wa mahindi umepungua kwa asilimia 5.6, mtama kwa asilimia 7.3, unga wa muhogo kwa asilimia 9.3, maharage kwa asilimia 9.2 na mihogo mibichi kwa asilimia13.2.

Baadhi ya wapiga picha jongefu wakiwa kazini wakati wa mkutano baina ya Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo (hayupo pichani) leo Jijini Dar es Salaam. Mfumuko wa bei wa Taifa umeshuka toka asilimia 3.9 mwezi Machi hadi kufikia 3.8 April. (Picha na: Frank Shija).

Kwesigabo aliongeza kuwa mfumuko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya mfumuko wa bei wa mwezi Aprili, 2018 umepungua hadi asilimia  3.73 toka asilimia 4.18 mwezi Machi na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 1.8 toka asilimia 2.0 mwezi Machi, 2018

Mfumuko wa Bei ambao hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.

172 thoughts on “Mfumuko wa Bei Washuka na Kufikia Asilimia 3.8

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama