Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Mpina Afuta Tozo Zote za Mifugo Zisizozingatia Sheria.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma baada ya kufika kijijini hapo kisha kuamuru wafugaji waliokamatiwa mifugo yao na kutozwa faini ya sh 50,000 kila ng’ombe warudishiwe kiasi cha sh. 30,000 kutokana na faini hiyo kutozwa kinyume cha sheria.

Na. John Mapepele – GCU Mifugo na Uvuvi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amefuta tozo ya faini ya shilingi elfu hamsini kwa kila Ng’ombe mmoja na ameuagiza Uongozi wa Wilaya ya Singida  kuwarudishia mara moja fedha wafugaji wote  walizotozwa faini kinyume cha Sheria  katika zoezi  la kukamata mifugo linaloendelea katika Hifadhi ya Msitu wa Jamii wa Mgori.

Waziri Mpina ametoa maelekezo hayo leo alipotembelea eneo la Hifadhi ya Msitu wa Jamii wa Mgori, kwenye Kijiji cha Handa na kuwaagiza Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma kupitia kwa Wakuu wa Wilaya ya Singida na Chemba  kushirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo kufika katika eneo hilo kabla ya tarehe15/12/2017 kushughulikia mipaka baina eneo la Singida na Handa kwa upande wa Wilaya ya Chemba  na migogoro ya wafugaji inayoendelea.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akimsikiliza kwa makini Mkazi wa Kijiji cha Handa wilayani Chemba, Jumanne Sadick kuhusu tatizo la mpaka kati ya Pori la Hifadhi ya Swagaswaga na Mgori ambapo Waziri Mpina aliagiza ifikapo Disemba 15 mwaka huu Katibu Mkuu Mifugo na viongozi wa Mkoa wa Singida na Dodoma kufika eneo hilo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akisoma stakabadhi ya malipo ya sh 50,000 kwa kila ng’ombe kinyume cha sheria aliyotozwa mfugaji wa Kijiji cha Handa, Tulway Bombo ambapo Waziri Mpina alitangaza kufuta maamuzi hayo na kuamuru wafugaji hao kurudishiwa fedha zao.

“Kama Waziri mwenye dhamana ya kushughulikia Sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini sipo tayari kuvunja Sheria kwa kuwakumbatia wahalifu wanaokiuka Sheria za nchi kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi, lakini pia wahalifu wanatakiwa kutozwa  faini kulingana  na Sheria na taratibu zilizowekwa. Utozaji wa faini ambao hauzingatii hili ni uvunjaji wa Sheria “ alisisitiza Mpina.

Waziri Mpina alisema utozaji wa faini wa shilingi 50,000/= toka shilingi 20,000/= za awali kwa kila Ng’ombe aliyekamatwa na shilingi 25,000/= kwa Mbuzi toka shilingi 5,000/= za awali haukubaliki na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Singida, Elias Tarimo kurudisha  shilingi 30,000/= kwa kila Ng’ombe ambazo zimetozwa  bila kufuata Sheria yoyote.

Baadhi ya wafugaji waliofika katika kijiji cha  Handa kulalamikia tozo  ya shilingi 50,000 kwa kila Ng’ombe  mmoja  walizotozwa  na Halimashauri ya Wilaya ya Singida ni  pamoja na Jerumani Waline aliyetozwa jumla ya shilingi 2,500,000/=, kwa idadi ya mifugo 66, Mabula Mwala aliyetozwa shilingi 1,950,000/= kwa idadi ya mifugo 45, Joel Tahan aliyetozwa jumla ya shilingi 1,000,000/= kwa idadi ya mifugo 31, Elizabeth Hamisi aliyetozwa shilingi 1,050,000/= kwa idadi ya mifugo 34,na Elizabethi Nyambi aliyetozwa jumla ya shilingi 350,000/= kwa idadi ya mifugo 8.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akimuuliza maswali Mwanasheria wa Halmashauri ya Singida, Fortunata Matinde juu ya sheria gani iliyotumika kutoza faini ya Sh. 50,000 kwa kila ng’ombe ambapo Waziri Mpina alifuta maamuzi hayo (kushoto) ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo) Dk Maria Mashingo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akiagana na wananchi wa Kijiji cha Handa wilayani Chemba mkoani Dodoma baada ya kutengua maamuzi yaliyofanywa na Halmshauri ya Wilaya ya Singida kutoza faini ya sh. 50,000 kila ng’ombe kinyume cha sheria aliyeko nyuma ya Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji bwana Jerumani Waline, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni kuainishwa kwa mipaka ya Kijiji cha Handa na Hifadhi ya Msitu wa jamii wa Mgori na eneo la kunyeshea maji  mifugo  ambapo alimuomba Waziri kulishughulikia suala hilo.

Waziri Mpina ameiagiza Halmashauri ya Singida kupitia mara moja tozo hizo na kuzipeleka kwenye Mamlaka husika ili zipitishwe na kuanza kutumika kwa taratibu zinazokubalika kisheria.

Pia amezitaka Halmashauri zote nchini kutojiingiza katika mtego wa kutoza  faini ambazo hazipo kisheria kwa kuwa  kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuagiza kuwa kuanzia sasa Halimashauri zote zinatakiwa kutoa  taarifa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pindi zinapotaka kuendesha operesheni za  mifugo ili kuwa na ufahamu wa pamoja baina ya Wizara na wadau wengine  hali ambayo itasaidia kuboresha operesheni hizo na kuondoa migongano isiyo ya lazima.

 Aidha amewataka Watendaji  kuwa makini wanaposhughulikia masuala  ya mifugo kwa kuhusisha  Sheria  mbalimbali za Sekta ya Mifugo ili kuondokana na migogoro isiyo  ya lazima kwa vyombo vya Serikali na kutolea mfano wa Uongozi wa Pori la Akiba  la Swaga Swaga ulivyowazuia Wakaguzi wa  Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia afya za mifugo iliyokamatwa  katika pori hilo, akasisitiza kuwa ni ukiukwaji wa sheria kwa kuwa sheria namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama  ya mwaka 2003, kipengele 26 (a)1 kinawapa uwezo Wakaguzi kuingia na kuchunguza  hali ya mifugo  mahali popote ili kuona afya za mifugo.

Alizitaja baadhi ya Sheria za Mifugo ambazo ni muhimu kuzizingatia wakati wa operesheni za mifugo kuwa ni pamoja na Sheria ya  Veternari Namba 16 ya Mwaka 2003, Sheria ya Tasnia ya Maziwa Namba  8 ya Mwaka 2004, Sheria ya Tasnia ya Nyama Namba 10 ya Mwaka 2006, Sheria ya Biashara ya Ngozi (The Hides, Skin and  Leather trade Act) Namba 18 ya Mwaka 2008, Sheria ya Ustawi wa Wanyama  Namba 19 ya Mwaka 2008 na Sheria ya Utambuzi, Usajili  na Ufuatiliaji Mifugo Namba 12  ya Mwaka 2010.

Sheria nyingine ni Sheria ya Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo Namba 13 ya Mwaka 2010, na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo namba 4 ya Mwaka 2012.

Akizungumzia ugomvi wa wafugaji kuingiza   mifugo katika Pori la Akiba la Swaga Swaga na Msitu wa Jamii wa Mgori, Waziri Mpina amesema  Viongozi wa Wilaya wanajukumu la kuyalinda maeneo hayo na wafugaji kuheshimu sheria za nchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Dkt. Mary Mashingo amesema  wataalamu wanatakiwa kushirikiana na kupanga mamna bora ya matumizi ya maeneo hayo ili kuleta tija kwa Sekta zote badala ya kuendelea na migogoro isiyoisha kila uchao.

“Wenzetu wa Ethiopia wamefanya vizuri katika kupanga na kutumia maeneo  kama haya,sisi kama Wizara tutahakikisha Sheria na Kanuni zinaboreshwa ili kuinua sekta ya Mifugo” alisisitiza Dkt. Mashingo.

Akitoa taarifa kwa Waziri kuhusu zoezi la kuondoa Mifugo na makazi katika eneo  hilo, Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amesema kwamba wameamua kufanya operesheni hiyo maalum baada ya  wafugaji hao kukataa kuondoka  katika eneo hilo  kuanzia mwaka 2010 ambapo walianza kuvamia na kufanya makazi,kulima mazao na kuchunga mifugo kinyume cha taratibu.

Alisema Wilaya iliamua kutoza  faini kubwa  kutokana na  hali ya wafugaji hao kuendelea na uvamizi na  kuendesha shughuli mbalimbali za ujenzi, ufugaji na kulima, hata hivyo alikiri kutofuata taratibu ya kuendesha zoezi hilo na kwamba watafuata taratibu za kisheria ili tozo hizo zipitishwe katika Mamlaka husika.

Aidha alisema operesheni hiyo imekuwa ikishirikisha  Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuwa wananchi wamekuwa wakitumia silaha kukataa kuondoka na kuchukuliwa mifugo yao hali ambayo imewafanya waendeshe operesheni hiyo kwa tahadhali  kubwa.

Amesema hadi sasa watu 32 wanashikiliwa na Polisi katika kituo cha Singida kutokana na zoezi la kuondoa mifugo linaloendelea, ambapo jumla ya nyumba 138 zimevunjwa na tozo za jumla shilingi 19,750,000/= zimekusanywa.

Mkuu wa Wilaya Tarimo amesema  jumla ya ng’ombe 386 walikamatwa na Halmashauri  lakini hadi sasa wameachiwa  baada ya wafugaji hao kulipa faini. Eneo la Pori la Mgori lina julma ya hekta 40000.

 

 

70 thoughts on “Waziri Mpina Afuta Tozo Zote za Mifugo Zisizozingatia Sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama