Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wizara ya Kilimo Yafanya Mapitio ya Sifa za Viongozi wa Vyama vya Ushirika

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe

 

Na Mathias CanalWizara ya Kilimo-Rukwa

Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sektaya Ushirika.

Dhana ya kuchagua viongozi wa ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika imepitwa na wakati hivyo kuna kila sababu ya kuchagua viongozi wenye weledi na utashi katika utendaji.

Hayo yameelezwa jana tarehe 8 Januari 2019 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakati akizungumza kwenye kikao kazi na maafisa wa Kilimo wa Wilaya za Mkoa wa Rukwa, Wadau mbalimbali wa Kilimo wakiwemo mawakala wa pembejeo, wasindikaji, wawakilishi wa vyama vya msingi vya ushirika na wakulima, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Alisema kuwa mfumo wa ushirika  ni nyenzo muhimu ambayo ukitumika vizuri itasaidia kuondoa  umaskini wa wakulima hapa nchini na utaimarisha uanzishwaji wa viwanda kuleta tija katika kilimo hivyo ni lazima kuwa na juhudi za makusudi kuwa na viongozi wenye weledi.

Katibu Mkuu huyo katika ziara yake mkoani Rukwa alitembelea maduka na maghala ya mbolea yanayomilikiwa na kampuni za ETG, YARA na PREMIER na kujionea hali halisi ya upatikanaji wa mbolea ambapo amepongeza utoshelevu wa mbolea uliopo mkoani humo.

Akizungumzia swala la masoko ya mazao ya wakulima Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ubora wa mazao ya wakulima ni suala la msingi kulizingatia ili kuweza kusaidia wakulima

kupata masoko ya uhakika na kujiongezea kipato, kwani mazao bora yana ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kuhusu Milipuko ya visumbufu vya mimea, Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ili kunusuru mazao ya wakulima nchini, hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa ili kuweza kudhibiti

wadudu wanaothiri mazao akiwemo Kiwavijeshi Vamizi (FAW).

Hivyo, alitoa rai kwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa na Makatibu Tawala wote nchini, kuwaagiza Maafisa Kilimo kufanya tathmini ya awali na kubaini maeneo ambayo kiwavijeshi

vamizi ameanza kuonekana ili Wizara kwa kushirikiana na halmashauri ziweze kuchukua hatua za kudhibiti milipuko ya kiwavijeshi vamizi kabla hajasambaa zaidi na kuleta athari kubwa.

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail