Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wizara ya Afya Yapata Bilioni 26.6 Kutoka Serikali ya Ujerumani

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la giz Dkt. Mike Falke akisaini mkataba wa makubaliano na serikali ya tanzania kupitia wizara ya afya katika kuimarisha afya ya msingi nchini, kushoto ni katibu mkuu wa wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula

Na. Catherine Sungura- Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesaini mkataba wa makubaliano wa miaka mitatu na serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kuimarisha afya ya msingi nchini.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa wizara yake imesaini mkataba huo na serikali ya Ujerumani katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo manne ambapo sekta hiyo itapata kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 26.6.

Katibu Mkuu Idara kuu Afya Dkt. Zainabu Chaula akisaini mkataba huo wa shilingi bilioni 26.6 kutoka Serikali ya Ujerumani, Halfa hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Wizara uliopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akimuonesha kitabu cha masuala ya mama na mtoto Bi. Vera Rosendahl mwakilishi kutoka Serikali ya Ujerumani

Dkt. Chaula amesema kwamba kwa mwaka huu wameweka makubaliano ili fedha hizo zitolewe kwa wakati mmoja na kuweza kutumia mfumo wa Force Akaunti kama walivyoweza kutumia kwenye ujenzi wa Vituo vya afya na Hospitali za Wilaya na Mikoa katika kuboresha sekta ya afya nchini.

“Tumeanza mahusiano tangu mwaka 1961, kuanzia  mwaka 2003 huu ni mkataba wa tano na mkataba wao ni wa miaka mitatu mitatu ambapo umejikita katika kuimarisha afya ya msingi katika halmshauri zetu katika vituo vya afya pamoja na zahanati”.

Dkt. Chaula alitaja maeneo yatakayonufaika na mkataba huo ni uhimarishaji wa taarifa, afya ya mama na mtoto, uzazi wa mpango, bima ya afya kwa akina mama wajawazito pamoja na utawala bora jinsi ya kutumia fedha hizi kulingana na kanuni na taratibu za nchi.

Viongozi wa Wizara na Serikali ya Ujerumani wakati wa mazungumzo ya pamoja katika kuboresha sekta ya afya

Mwakilishi wa Serikali ya Ujerumani Bi. Vera Rosendahl akiongea wakati wa kusaini mkataba kati ya nchi yake na Serikali ya Tanzania

Katibu Mkuu Idara kuu Afya Dkt. Zainabu Chaula na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la GIZ Dkt. Mike Falke wakibadilishana mikataba hiyo mara baada ya kusaini

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula na baadhi ya viongozi kutoka shirika la GIZ la Serikali ya Ujerumani mara baada ya kusainiana mkataba

“Huu ni muendelezo wa mkataba wa miradi mingi ambayo tumeifanya katika kuboresha sekta ya afya, kama mnavyokumbuka hadi sasa hivi tumeshafanyia ukarabati wa vituo vingi vya afya ambapo tuna vituo 470 ambavyo vimeshafanyiwa ukarabati  tangu mwaka 2017 katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya.

Aidha, Dkt. Chaula alisema Serikali iliwekeza shilingi bilioni mia moja na milioni mia tano katika hospitali za halmashauri.

“Zamani hawa wenzetu walikua wakitumia wakandarasi wao na pesa wanakaa nazo hivyo tumekaa nao na kukubaliana kama fedha hizi watazitoa kwa wakati mmoja ili tuweze kuzisimamia kama tulivyofanya kwenye vituo tulivyoanza ili kuweza kutekeleza kwa umakini na kupata matokeo makubwa katika kipindi hiki” . Amesema Dkt. Chaula.

Kwa upande wa hali ya uzazi, mama na mtoto Katibu Mkuu huyo alisema hivi sasa inakaribia asilimia 80 ya akina mama wajawazito wanajifungulia kwenye vituo vya afya tofauti na zamani ambapo kulikuwa na changamoto kubwa kwani wengi walikua wanajifungulia majumbani kwa asilimia 39 na kufuatia na asilimia 59 hii ni kutokana na kuboreshwa kwa  vituo vya afya pamoja  na mikakati mbali mbali ya kuhakikisha akina mama wote wanajifungulia kwenye vituo vya afya.

81 thoughts on “Wizara ya Afya Yapata Bilioni 26.6 Kutoka Serikali ya Ujerumani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama