Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Mkuu Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Vituo vya Kupoza Umeme kwa Mikoa Minne

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia) na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) wakipongezana mara baada ya Waziri Mkuu, kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo Misuna, wilayani Singida, Mkoa wa Singida. Kituo hicho kinaongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Na: Teresia Mhagama, WN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka Jiwe la Msingi katika  mradi wa upanuzi wa vituo vinne vya kupoza umeme vinavyoongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400 katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga.

Hafla hiyo ilifanyika tarehe 5 Oktoba, 2019 mkoani Singida na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifunua kitambaa kuashiria uwekaji jiwe la msingi katika mradi upanuzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo Misuna, wilayani Singida, Mkoa wa Singida. Kituo hicho kinaongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Baadhi ya wafanyakazi katika mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo Misuna, wilayani Singida, Mkoa wa Singida wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo hicho kinachoongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini(REA), Mhandisi Amos Maganga na watendaji kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA).

Waziri Mkuu, alisema kuwa, tukio hilo linaashiria pia uzinduzi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida, Manyara, Arusha, Namanga hadi Isinya nchini Kenya (KTPIP) ambao tayari upo kwenye hatua za ujenzi.

Aliongeza kuwa, kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha gridi ya Taifa kuwa na uwezo mkubwa wa usafirishaji umeme na kuwezesha nchi kuwa na umeme wa uhakika, unaotosha mahitaji  na unaotabirika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua mara baada ya kuwasili katika eneo la Misuna wilayani Singida ili kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme. Kituo hicho kinaongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Baadhi ya viongozi, wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakandarasi pamoja na wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo cha kupoza umeme kilichopo Misuna, wilayani Singida, Mkoa wa Singida. Kituo hicho kinaongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Alisema, Serikali inaendelea na jitihada za utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ukiwemo mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) kwani lengo ni kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 na kusambaza umeme kwenye maeneo yote nchini.

Waziri Mkuu, vilevile aliipongeza Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kwa usimamizi thabiti wa miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji umeme vijijini ambapo ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu jumla ya Vijiji 8,102 vimesambaziwa umeme kati ya vijiji 12,268.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alieleza kuwa mradi wa upanuzi wa vituo hivyo vya kupoza umeme ni wa Awamu ya Pili kwani Awamu ya kwanza ilijumuisha ujenzi wa njia kuu ya kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyaga, pamoja na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kwa msongo wa Kv 220 kwenye miji ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga na ulikamilika Disemba 2016.

Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua akizungumza na wananchi wa Misuna wilayani Singida kabla ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo katika eneo hilo. Kituo hicho kinaongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia, mbele) na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto, mbele) na viongozi mbalimbali wakipiga makofi mara baada ya Waziri Mkuu kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo Misuna, wilayani Singida, Mkoa wa Singida. Kituo hicho kinaongezewa nguvu ya umeme kutoka kV 220 hadi kV 400.

Aliongeza kuwa mradi huo wa awamu ya kwanza ulisambaza umeme kwenye vijiji 121 vilivyopitiwa na miundombinu ya umeme na kwa mradi huu wa Awamu ya Pili, jumla ya vijiji 19 vitakavyopitiwa na miundombinu ya umeme kutoka Singida, Manyara hadi Arusha vitasambaziwa umeme.

Alisema kuwa gharama zitakazotumika kwenye ujenzi wa vituo hivyo vinne vya kupoza umeme ni Dola za Marekani milioni 120  na Kituo cha Singida kinatarajiwa kukamilika mwezi Februari mwaka 2020.

29 thoughts on “Waziri Mkuu Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Vituo vya Kupoza Umeme kwa Mikoa Minne

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama