Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Mkuu aridhishwa ujenzi TB III

Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale akisoma taarifa ya Ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), hivi karibuni alipowasili kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema hivi karibuni kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi wa Jengo ka Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB III), wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Mhe. Majaliwa amesema amefarijika kusikia ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia 95.05, ambapo imebaki asilimia 4.5 pekee kukamilika.

“Nawapongeza wakandarasi, Tanroads na wote mliopata ajira ya ujenzi wa jengo hili naamini sasa mmekuwa wataalam hodari, kwani jengo ni zuri, linavutia na lenye ubora nimeona maeneo muhimu pale pa kuondokea abiria, sehemu ya kupokelea mizigo na kwenye madaraja ambapo kote nimefarijika kwa kiasi kikubwa ujenzi unakwenda vyema,” amesema Mhe. Majaliwa.

Amesema mbali na ujenzi huo pia amefurahishwa na ukuta unaotambulika kama “Wall of Tanzania” ambao unaonyesha picha za vivutio mbalimbali ukiwemo mlima mrefu Barani Afrika, Mlima Kilimanjaro, Bahari, Majahazi, minazi, wamasai, wanyama Twiga, Tembo, Pundamilia, Nyumbu, Simba na Chui, ambao hutambulisha wageni kuwa tayari wamewasili Tanzania na wataweza kuona vivutio hivyo, ambavyo ni alama na nembo ya nchi.

Kiongozi Mkuu wa Timu ya Wataalam wa Ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Julius Ndyamukama (aliyenyoosha mkono) akimuonesha Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ukumbi wa abiria wanaoondoka katika jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipotembea hivi karibuni.

“Hizi picha ni nembo ya Kitanzania, na hapa zimekaa sehemu nzuri sana kila mgeni anapowasili na kufika eneo hili la kuchukulia mizigo anaona kweli amefika Tanzania kwani zinawakaribisha wageni, na hii ni faraja kwa kuwa jitihada za serikali za kuleta maendeleo zinafanyika vyema,” amesema Mhe. Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa pia amekuwa na faraja kubwa kusikia jengo hilo litaweza kuhudumia abiria milioni sita (6) kwa mwaka, na kwa majengo yote likiwemo Jengo la Kwanza na la Pili jumla yataweza kuhudumia abiria milioni nane (8) kwa mwaka, ambapo pia kumekuwa na miundombinu kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiangalia aina ya viti vya abiria vitakavyotumika kwenye Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) alipotembelea hivi karibuni. Kulia kwa Waziri Mkuu ni Bi. Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Ilala na wa pili kushoto ni Mhandisi Julius Ndyamukama, akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.

Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bw. Vedastus Fabian (watatu kulia) wakitoka katika jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) mara baada ya ziara ya waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kumalizika hivi karibuni.

Hatahivyo, ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ianze kukamilisha  taratibu za kuanza kutumika kwa jengo hilo, ili mkandarasi anapolikabidhi kwa serikali ifikapo tarehe 31 Mei, 2019 lianze kutumika mara moja.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao ndio wasimamizi wa ujenzi Mhandisi Patrick Mfugale awali alimweleza Mhe. Majaliwa kuwa ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia 95.05, ambapo eneo la maegesho ya ndege linaweza kuegesha ndege 19 za darala C, na 11 daraja E na jengo linaweza kuhudumia abiria 2,800 kwa saa muda ambao abiria ni wengi.

Hatahivyo, Mhandisi Mfugale amemhakikishia Mhe,. Majaliwa kuwa ujenzi huo utakamilika kwa wakati na viwango vilivyowekwa, amesema jengo hilo litakabidhiwa kwa serikali tarehe 31 Mei, 2019.

13 thoughts on “Waziri Mkuu aridhishwa ujenzi TB III

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *