Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Kairuki Awatoa Hofu Wawekezaji Nchini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiangalia maji yanayozalishwa na kiwanda cha ASANTE wakati wa ziara yake kiwandani hapo wa kwanza kulia ni Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Bi. Katrini Mwimbe.

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia  Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki amewatoa hofu wawekezaji na wafanyabiashara juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Akizungumza  mwishoni mwa wiki jijini Dodoma, wakati wa ziara yake  ya kukagua shughuli za uzalishaji katika viwanda vinavyozalisha mvinyo kikiwemo DOMIYA ESTATE kinachozalisha  vinywaji vikali na baridi kama  soda, maji na chai baridi aina ya ASANTE na kiwanda  cha Alko Vintages Co. Ltd amesema kuwa Serikali ina mipango na mikakati ya kuhakikisha kuwa kuna  mazingira bora ya uwekezaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiangalia moja ya mvinyo aina ya presidential reserve white – passito unaozalishwa katika kiwanda cha DOMIYA kilichopo Jijini Dodoma alipotembelea kiwandani hapo.

“Serikali inatambua changamoto mnazopitia na imeweka mikakati ya kuhakikisha inazitatua ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya uwekezaji nchini inayolenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji,”alisema Waziri Kairuki

Amesema, changamoto ambazo wawekezaji wamekuwa wakikabiliana nazo zinaendelea kutatuliwa ikiwa ni pamoja na; utitiri wa kodi, ukosefu wa maji ya uhakika, ubovu wa miundombinu ya barabara, gharama kubwa za uzalishaji, uzalishaji duni kwa ubora na wingi wa zabibu, ukosefu wa aina mabalimbali za zabibu.

Mhandisi wa umeme wa kiwanda cha kuzalisha vinywaji baridi cha ASANTE, Alpha Mbennah akitoa maelezo kuhusu mitambo inayotumika katika uzalishaji wa hatua za mwisho kwa Waziri wa Nchi Ofisi wa Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea kiwandani hapo Jijini Dodoma.

Changamoto nyingine walizobainisha ni; ugumu wa kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika zabibu, ukosefu wa utaalamu katika kilimo cha zabibu, pamoja na uwepo wa bidhaa zisizo na ubora sokoni.

Akijibu changamoto hizo, Waziri Kairuki aliwatoa hofu kwa kuainisha maeneo muhimu yaliyofanyiwa maboresho ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa tozo na kodi zaidi ya 168 nchini, kuendelea kuboresha miundombinu muhimu ikiwemo barabara zinazosimamiwa na TARURA,  kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme na maji ili kila mwekezaji na mfanyabiashara anufaike na kuwekezaji kwake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akioneshwa na kupewa maelezo kuhusu mtambo wa kuzalisha mvinyo kutoka kwa Mhandisi wa Kemikali na Mchakato tija wa kiwanda hicho, Daniel Mollel wakati wa ziara yake katika kiwanda cha kuzalisha mvinyo cha DOMIYA.

Aidha Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo  cha Uwekezaji nchini  inaendelea kuandaa mpango wa kuteua mabalozi kwa lengo la kuvutia wawekezaji kama ilivyo  katika sekta nyingine ikiwemo utalii.

“Tumeendelea na hatua za awali za kuanzishwa kwa mpango wa kuwa na mabalozi watakao tangaza masuala ya uwekezaji nchini, hii ni pamoja na kushirikisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuona namna ya kupata mabalozi hao watakaofikia taifa na nje ya Nchi,”alisisitiza Waziri Kairuki

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki atoa majumuisho ya ziara yake katika eneo la uzalishaji la DOMIYO ESTATE lililotengwa kwa ajili ya kuzalisha mvinyo, vyumba vya kulaza wageni, kiwanda cha vinywaji baridi mara baada ya ziara ya kukagua shughuli zinaoendelea katika eneo hilo wakati wa ziara yake kijiji cha Chinyoya Dodoma.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashauri wawekezaji kuvitumia vyema vyombo vya habari katika kutoa elimu na kujitangaza ili kuendelea kuwa na soko la uhakika kwa kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Naye Mchumi Mkuu kutoka Idara ya Uwekezaji Bw. Francis Mollay, alibainisha baadhi ya jitihada za kuhakikisha wawekezaji wananufaika na uwekezaji wao pamoja na uwepo wa sheria na kanuni zinazobainisha namna bora ya kuboresha mazingira yao ili kuwa na maendeleo katika sekta zote.

“Tunaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kupitia sheria na sera zinazohusiana na kodi mbalimbali ili kutatua changamoto za kikodi zilizopo,”alieleza Mollay.

Kwa upande wake Mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Alko Vintages Bw. Archard Kato alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji na kutoa rai kwa vijana kutumia fursa zilizopo katika kilimo hasa cha zabibu kwa kuonesha nia na uthubuti ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

“Vijana lazima mjiamini na kuwa na uthubutu katika kuanzisha biashara ili kuingia kwenye sekta ya uwekezaji, hakikisha una maono au jambo linalokuvutia na weka mikakati ya kulifikia.Hakikisha unajaribu wazo ulilonalo na kuwatumia walioweza katika hilo, utayaona manufaa kama kijana,”alisema Kato.

Kiwanda kingine alichotembelea ni Alko Vintages Co. Ltd kinachozalisha mvinyo wa aina mbalimbali ikiwemo Dompo, Altar, St. Mary’s, Image, Rose na Klymax viliyopo katika Wilaya ya Dodoma Mjini mkoani Dodoma.

24 thoughts on “Waziri Kairuki Awatoa Hofu Wawekezaji Nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama