Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wawekezaji wa Ndani, Nje Wanathaminiwa Sawa – Serikali

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akizungumza na Waandishi wa Habari masuala ua uwekezaji walipokutana nao wakati wa kongamano la kujadili masuala hayo kwa wawekezaji wa Kimarekani, kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, kushoto kwake ni Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Dkt. Inmi Patterson.

Na.Mwandishi Wetu –MAELEZO.

Serikali imesema wawekezaji wa nje na wale wa ndani ya nchi wanapewa heshima na thamani sawa sawa na hakuna mahala popote ambapo kumekuwa na ubaguzi wa kiuwekezaji wala wa utoaji wa vibali ama urasimu wa aina yoyote ambao unawakwamisha.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwezeshaji  Angelah Kairuki alipozungumza kwenye mjadala maalum ulioandaliwa na ubalozi wa Marekani kwa kushirikiana na chama cha wafanyabiashara wa marekani hapa nchini, uliofanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kairuki amesema, serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kuboresha mazingira ya uwezeshaji kwa wawekezaji wa ndani na wale wa nje ya nchi na dhamira yake ni kuendelea kuwasaidia ili wafanya biashara na uwekezaji wao bila vikwazo vyovyote.

“Dhamira ya dhati ya Mh.Rais katika kusimamia na kuendeleza wawekezaji imejidhihirisha bayana na hivi karibuni tu aliwaalika wafanyabiashara na wawekezaji Ikulu Jijini Dar es Salaam ili kuwasikiliza na kuwasaidia kutatua kero zao” Alisema Waziri Kairuki.

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kongamano hilo, wa pili kutoka kushoto waliokaa ni Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Dkt. Inmi Patterson.

Amesema kwakuwa sasa mazingira ya uwekezaji na biashara yamewezeshwa Serikali inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na wa  nje ya nchi kuja kuwekeza hapa nchini, pia amewataka kutoa taarifa pale ambapo wanaona taratibu hazijakaa sawa ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka kwani duniani kote wawekezaji na wafanyabiashara ndio wanachangia kwa kiasi kikubwa katika kupatikana kwa mapato.

Amesema juhudi za Rais Magufuli za kuendeleza uwekezaji hazikuanza leo ndio maana akaamua kumteua yeye kama Waziri  anayeshughulikia  uwekezaji, hii inaonyesha namna anavyojali uwekezaji na yeye na timu yake akiwemo Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamejipanga kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji wenye tija.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Palamagamba Kabudi amesema, kila mahala serikali inaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ya reli, barabara bandari na hata usafiri wa anga ili kurahisisha uwekezaji hapa nchini.

“Katika kulisimamia hili serikali pia imeendelea kudhibiti vitendo vya rushwa na ufisadi,lakini pia imeendelea kuondoa urasimu usio wa lazima ambao unarudisha nyuma juhudi za kukuza uwekezaji hapa nchini” Alisema Prof.Kabudi.

Aidha Prof.Kabudi amesema serikali pia imeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwaajili ya kuiwezesha kuendelea kujenga miradi mikubwa ya kimkakati, lakini pia imeendelea kuhakikisha inawaelimisha wawekezaji kwamba juhudi za kukusanya mapato hazina lengo la kumuumiza mwekezaji na mfanyabiashara.

Naye Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Dkt.Inmi Patterson majadiliano hayo yamekuja wakati muafaka mabapo serikali ya Tanzania inaendeleza jitihada za kuimarisha uchumi na pia kuwawezesha wawekezaji na wafanyabiashara.

 

227 thoughts on “Wawekezaji wa Ndani, Nje Wanathaminiwa Sawa – Serikali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama