Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wauzaji wa Mbolea Watakiwa Kuzingatia Ubora

Na Ismail Ngayonga.

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Uthibiti wa Mbolea Nchini (TFRA) imewaagiza  Wafanyabiashara na wauzaji wa mbolea nchini kuzingatia ubora wa viwango vya bidhaa hiyo na kuepuka kuwauzia wakulima mbolea isiyokidhi viwango vya ubora vilivyotolewa na Shirika la Viwango Nchini (TBS).

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uthibiti wa Mbolea Nchini (TFRA), Lazaro Kitandu wakati wa mahojiano ya kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO na kurushwa hewani na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC).

Kitandu alisema tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2012, taasisi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti kuenea kwa mbolea feki, ambazo zimekuwa hazileti tija iliyokusudiwa kwa Wakulima wengi nchini.

Aliongeza kuwa baadhi ya wauzaji wa mbolea nchini wamekuwa wakiuza mbolea katika utaratibu usioruhusiwa kisheria ikiwemo ufunguaji wa mifuko na kuifanya bidhaa hiyo kuuzwa mfano wa chumvi au sukari jambo ambalo limekuwa likipoteza ubora wa bidhaa hiyo nchini.

“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wauzaji na wafanyabiashara kuhusu kuzingatia sheria, na wakati mwingine tumekuwa tukifanya ukaguzi wa kushtukiza na tayari tumewabaini wafanyabiashara wengi na kuwachulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafutia leseni na kuwatoza faini ya Tsh. Milioni 8” alisema Kitandu.

Aidha alisema kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi wa mbolea zote za viwandani  zinazoingizwa nchini kuanzia hatua ya utengenezaji, usafirishaji na utunzaji wa bidhaa hiyo katika maghala ili kuthibiti ubadilishaji wa  thamani yake pindi inapokuja kutumiwa na wakulima.

Kwa mujibu wa Kitandu alisema TFRA kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya imekuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara kwa kutumia Wataalamu wake waliopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa Mkulima wa Tanzania anapata bidhaa iliyokidhi kiwango cha ubora.

Akifafanua zaidi Kitandu alisema ni wajibu wa Wafanyabiashara kuzingatia sheria na. 9 ya mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2011 katika uagizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa ya mbolea.

“Asilimia 90 ya mbolea yote inaagizwa kutoka nje ya nchi, ikiwemo China, Ukraine, Japan, Norway, Marekani, Urusi na Morocco, hivyo tunawajibika kuhakikisha kuwa mbolea hizo zinakuwa na ubora unaokidhi viwango” alisema Kitandu.

Aliongeza kuwa kiwango cha mahitaji ya mbolea nchini kimeongezeka nchini ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, ambapo kwa sasa kiwango cha mahitaji kimefikia tani 380,000 kwa msimu, ambapo lengo la Serikali ni kuzidisha matumizi ya mbolea za ndani ili kuwapunguzia gharama wakulima.

Kitandu alisema katika kuwekea mkazo matumizi ya mbolea ya ndani, Serikali tayari imefanya mazungumzo na wawekezaji mbalimbali ili kujenga viwanda katika Mikoa inayozalisha gesi nchini ambayo ni Mtwara na Lindi.

 

One thought on “Wauzaji wa Mbolea Watakiwa Kuzingatia Ubora

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *