Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watuhumiwa 29 wa Mauaji Njombe Wakamatwa

 

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO,DODOMA.

Watu 29 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya utekaji na mauaji ya watoto Mkoani Njombe.

Akiwasilisha bungeni leo Jijini Dodoma taarifa ya Serikali kuhusu mauaji hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola amesema Serikali imeshachukua hatua mbalimbali katika kutatua na kuzuia matukio hayo sanjari na kutoa maelekezo ya hatua za kupambana na uhalifu huo ikiwemo kuwatia mbaroni watuhumiwa.

“Mpaka sasa hatua zilizochukuliwa na Serikali zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 29 kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano zaidi na kazi bado inaendelea” ameongeza Waziri Lugola.

Mhe. Lugola amebainisha kuwa,  hivi karibuni kumejitokeza matukio yasiyo  ya kawaida ya utekaji na mauaji ya watoto yaliyokuwa yakihusishwa na imani potofu za kishirikina katika Mkoa wa Njombe.

“Kufuatia matukio hayo hadi sasa watoto saba wa umri chini ha miaka 16 wameripotiwa kuuawa, mmoja kujeruhiwa na wawili kupotea na badae kuonekana, matukio haya yametokea  katika maeneo ya Ikando, Matembwe, Mjimwema, Msitu wa Sekondari ya Njombe, Lukosa, Sido na Mfekere,” ameeleza Waziri Lugola.

Akifafanua zaidi, Lugola amesema kuwa, mbali na juhudi za Serikali, Jeshi la Polisi kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe imechukua hatua mbalimbali kuzuia aina hiyo ya uhalifu kwa kutumia timu ya wataalamu wa upelelezi kuvisaidia vyombo vya dola kuchunguza matukio hayo.

Pia kutumia falsafa ya ulinzi shirikishi wa jamii kwa kutoa elimu mashuleni kwa walimu ili kuweza kuwaelimisha wanafunzi kuongeza umakini katika mienendo yao, kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa wazazi na wananchi kwa ujumla juu ya elimu ya ulinzi na usalama, vikao na waganga wa kienyeji, viongozi wa dini, Wazee wa Mila, Viongozi wa Kata pamoja na kufanga doria na misako kwenye maeneo mbalimbali ya misitu na nyumba za kulala wageni zilizopo pembezoni, ni mbinu zilizotumika kuzuia vitendo hivyo.

Hata hivyo, Mhe. Lugola ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na matukio hayo na itikadi za kisiasa, imani za kidini au shughuli za kibiashara.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali itachukua hatua kwa wale watakaojihusisha na vitendo vya usambazaji wa taarifa za kichochezi mitandaoni hivyo amewaasa Watanzania kuacha kusambaza taarifa za uzushi mitandaoni  kwa nia yoyote ile kwani ni takwa la Sheria ya Mtandao.

Mbali na hayo amesema kuwa, Serikali itahakikisha wote waliohusika na mauaji wanaendelea kusakwa, kuhojiwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria bila kujali nafasi zao katika jamii.

Hivi karibuni yamajitokeza matukio ya utekaji na mauaji ya watoto wadogo Mkoani Njombe, jambo ambalo limezua taharuki mkoani humo na nchini kote kwa ujumla.

(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *