Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watakiwa Kujitokeza kwa Wingi Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Luhumbi akizungumza na Waandishi wa Habari leo mkoani humo kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo.

Na Veronica Kazimoto

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara na wananchi wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi katika Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko, changamoto, maoni pamoja na kupata elimu ya masuala ya kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ujumla.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mhandisi Robert Luhumbi amesema kuwa, wafanyabishara na wananchi watumie fursa ya kampeni hii itakayomalizika tarehe 13 Aprili, 2018 kupata elimu sahihi ya masuala ya kodi na tozo mbalimbali.

“Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote wa mkoa huu hususani wale wanaoishi katika maeneo ya Masumbwe, Ushirombo, Rulembela, Katoro, Lunzewe, Namonge, Nyanghw’ale, Bwanga na Muganza kujitokeza kwa wingi ili waweze kujifunza, kupata huduma na kutoa maoni yao kwa watalaam wetu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kuyatolea ufafanuzi na kuyafanyia kazi,” amesema Mhe. Luhumbi.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita akizungumza wakati wa mkutano wa Waandishi wa Habari mkoani humo kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo.

Kiongozi wa timu ya watalaam kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Maternus Mallya akizungumza wakati wa mkutano wa Waandishi wa Habari mkoani Geita kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo. (Picha na Benedict Liwenga).

Nae Meneja wa TRA mkoani hapa, James Jilala amesema kuwa, lengo kuu la kufanya kampeni hii maalumu ni kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Kampeni hii ni mwendelezo wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi iliyofanyika nchi nzima kuanzia tarehe 5 hadi 9 Machi, 2018 katika ngazi ya mkoa. Kutokana na matokeo ya kampeni ile mkoani hapa, tumeona ni muhimu tuwe na kampeni nyingine maalumu ambayo inafanyika maeneo mbalimbali katika wilaya zetu tofauti na ile ya kwanza iliyofanyika Geita mjini tu,” amefafanua Jilala.

Kwa upande wake kiongozi wa timu ya watalaam kutoka TRA Makao Makuu Maternus Mallya ameeleza kuwa, timu yake imejipanga vizuri na tayari kazi imeanza kufanyika katika vituo vyote vilivyotengwa kwa ajili ya kampeni hiyo.

“Hapa ninapozungumza, wenzangu wako kwenye maeneo husika wanaendelea kufanya kazi. Hivyo, kama alivyosema Mhe. Mkuu wa Mkoa, nami natoa rai kwa wananchi wote mkoani hapa, kujitokeza kwa wingi ili waweze kukutana na watalaam wetu kwa ajili ya kupata huduma na elimu ya mlipakodi,” amesema Mallya.

Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani Geita imeanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara na wananchi watasajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kuelimishwa kuhusu ulipaji wa Kodi ya Majengo kwa njia ya kieletroniki.

 

70 thoughts on “Watakiwa Kujitokeza kwa Wingi Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *