Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watakaoshindwa Kufuata Muongozo wa Afya Michezoni Kuchukuliwa Hatua Kali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na Waandishi wa Habari katika uwanja wa Nyamagana uliopo mkoani Mwanza

Na Kelvin Kanje – Mwanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amewataka watakaoshindwa  kufuata muongozo wa afya michezoni wachukuliwe hatua kali.

Dkt. Abbasi ametoa agizo hilo jana katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo aliwaeleza wadau wa michezo kuwa Serikali imechukua uamuzi mgumu wa kufungua michezo yote  na tayari ratiba za mechi mbalimbali katika Ligi Kuu ya Soka nchini imetoka na timu zimeanza mazoezi, vilevile Serikali imetoa ruksa kwa mashabiki watakaotaka kuhudhuria  viwanjani waruhusiwe kwa taratibu maalamu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na uongozi wa uwanja wa CCM Kirumba, Mkoani Mwanza. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Yusuf Singo

Akikagua utayari wa viwanja vya soka kabla ya kuanza kwa ligi, Dkt. Abbasi amesisitiza kuzingatiwa kwa Muongozo huo ikiwemo mashabiki na wachezaji kunawa kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi kabla ya kuingia viwanjani, kupimwa joto, mashabiki kukaa kwa kuachiana mita moja na kusisitiza yeyote atakayekiuka taratibu hizo atachukuliwa hatua stahiki ikiwemo viwanja husika kufungiwa kutumika kwa ligi.

“Tumefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wake na wadau mbalimbali na wote wako tayari kuhakikisha yale yote ambayo Serikali imeagiza kwenye muongozo yanazingatiwa,” alisema Dkt. Abbas.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na uongozi wa uwanja wa Gwambina, uliopo katika Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza nakuendelea kusisitiza umakini katika utaratibu wa kuendesha michezo. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara hiyo,  Yusuf Singo.

Katika hatua nyingine, akiwa katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza na baadaye mkoani Shinyanga, Dkt. Abbasi amewapongeza wadau binafsi waliojenga viwanja vya Gwambina, Mwadui Complex na uwanja mwingine mpya wa Shinyanga Mjini.

“Uwekezaji huu ni mkubwa na umechangia juhudi za Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya michezo namwagiza Mkurugenzi wa Michezo awaletee wataalamu wetu ili washirikiane nanyi utaalamu katika baadhi ya maeneo hasa katika utunzaji wa nyasi za viwanja,” aliagiza.

Wachezaji wakifanya mazoezi katika uwanja wa CCM Kirumba uliopo mkoani Mwanza ikiwa ni maandalizi ya mechi zitakazofanyika katika uwanja huo hivi karibuni.

Katika ziara hiyo Dkt. Abbasi ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Yusuf Singo na kati ya viwanja walivyovikagua ni cha CCM Kirumba na Nyamagana.

 

19 thoughts on “Watakaoshindwa Kufuata Muongozo wa Afya Michezoni Kuchukuliwa Hatua Kali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama